Mjumbe Wa UN: Hali ya Burundi inaboreka
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i51673-mjumbe_wa_un_hali_ya_burundi_inaboreka
Mjumbe maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Burundi, Michel Kafando amesema hali ya kisiasa nchini humo imeanza kutia matumaini wakati huu ambapo taifa hilo linajiandaa kufanya uchaguzi mkuu hapo mwakani.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Feb 20, 2019 07:53 UTC
  • Mjumbe Wa UN: Hali ya Burundi inaboreka

Mjumbe maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Burundi, Michel Kafando amesema hali ya kisiasa nchini humo imeanza kutia matumaini wakati huu ambapo taifa hilo linajiandaa kufanya uchaguzi mkuu hapo mwakani.

Kafando alisema hayo Jumanne mjini New York, Marekani wakati akihutubia wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa waliokutana kujadili Burundi na kupokea taarifa ya Katibu Mkuu kuhusu taifa hilo la Maziwa Makuu.

Ametolea mfano hatua iliyotajwa ya aina yake ya kusajiliwa tarehe 14 mwezi huu CNARED, ambacho ni chama cha  upinzani kinachoongowa na Agathon Rwasa, hatua ambayo itawezesha chama hicho kushiriki kwenye uchaguzi mkuu mwakani.

Kafando amesema  hatua hiyo pamoja na ile ya Rais Pierre Nkurunzinza ya kurejelea tena mwezi Disemba mwaka jana kuwa hatowania tena nafasi ya urais wakati wa uchaguzi mkuu mwakani, ni ishara dhahiri ya kupanuka kwa uwanja wa demokrasia nchini humo.

Akihutubia kikao hicho, Mwakilishi Maalum wa Muungano wa Afrika kwenye Umoja wa Mataifa, Fatima Kyari Mohammed naye ameunga mkono kuwepo kwa utulivu kwenye hali ya siasa nchini humo kuelekea uchaguzi mkuu mwakani. Hatua hiyo ni pamoja na kuanzishwa kwa tume huru ya taifa ya uchaguzi.

Rais Pierre Nkurunziza wa Burundi

Naye Mwakilishi wa kudumu wa Burundi kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Albert Shingiro aliwahutubia wajumbe wa Baraza la Usalama ambapo alisema ni wazi kuwa kuna maendeleo makubwa katika mchakato wa kisiasa nchini Burundi akisema kuwa serikali imeanzisha mifumo ya kuhakikisha uchaguzi mkuu unafanyika kwa amani na utulivu, sambamba na Tume huru ya Taifa ya Uchaguzi ambayo tayari inafanya kazi.

Hali kadhalika amesema tayari kuna mazungumzo baina ya vyama vya upinzani kwa mujibu wa utaratibu wa Kayanza na kwamba Burundi imejizatiti kuliko wakati mwingine wowote ule kusogeza mbele haki za binadamu.