Maandamano yaendelea Sudan, wananchi wamtaka al Bashir ang'atuke
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i51726-maandamano_yaendelea_sudan_wananchi_wamtaka_al_bashir_ang'atuke
Askari wa usalama wa Sudan wametumia gesi ya kutoa machozi kukabiliana na mamia ya watu walifanya maandamano leo dhidi ya serikali ya nchi hiyo baada ya Swala ya Ijumaa.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 22, 2019 12:39 UTC
  • Maandamano yaendelea Sudan, wananchi wamtaka al Bashir ang'atuke

Askari wa usalama wa Sudan wametumia gesi ya kutoa machozi kukabiliana na mamia ya watu walifanya maandamano leo dhidi ya serikali ya nchi hiyo baada ya Swala ya Ijumaa.

Maandamano kama hayo yamefanyika katika mji wa Omdurman nje kidogo ya Msikiti wa Al-Sayed Abd al-Rahman al-Mahdi wenye mfungamano mkubwa na chama cha upinzani cha Umma na ni sehemu ya maandamano yanayofanyika karibu kila siku nchini Sudan dhidi ya serikali ya Rais Omar al Bashir.

Waandamanaji hao wamesisitiza udharura wa kuondolewa madarakani utawala wa miongo kadhaa wa Rais Omar al Bashir.

Maandamano ya baada ya Swala ya Ijumaa ya leo nchini Sudan yamefanyika siku moja baada ya maafisa wa polisi kuwatia mbaroni viongozi waandamizi wa vyama vya upinzani.

Chama cha Congress cha Sudan kimetangaza kuwa, vinara kumi wa vyama mashuhuri vya upinzani nchini humo wamekamatwa kabla ya kuanza maandamano mapya katika mji mkuu Khartoum.  

Wasudan wanamtaka al Bashir aondoke madarakani

Miongoni mwa viongozi wa upinzani waliotiwa mbaroni ni Naibu Mwenyekiti wa chama cha Umma, Mariam Sadiq al-Mahdi, Katibu Mkuu wa chama hicho Sara Naqdallah na kinara wa Chama cha Kikomunisti Mokhtar al-Khatib.

Sudan imekuwa ikisumbuliwa na wimbo la malalamiko na maandamano ya wananchi tangu tarehe 19 Disemba mwaka jana wanaolalamikia hali mbaya ya kiuchumi na ongezeko la bei za bidhaa hususan mkate na nishati.

Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International linasema kwamba watu karibu 60 wameuawa hadi sasa katika maandamano hayo.