Waangalizi: Makumi ya watu wameuawa Nigeria katika machafuko yanayohusiana na uchaguzi
Makumi ya watu wameuawa katika wimbi la machafuko yanayohusiana na uchaguzi wa rais na bunge nchini Nigeria, wakati nchi hiyo inasubiri kutangazwa matokeo ya uchaguzi huo.
Hayo ni kwa mujibu wa makundi ya asasi za kiraia za waangalizi wa uchaguzi huo uliofanyika siku ya Jumamosi.
Chumba cha Hali ya Mambo (Situation Room), kinachowakilisha makundi na asasi zaidi ya 70 za kiraia kimetangaza leo kuwa, machafuko yanayohusiana na uchaguzi yamesababisha vifo vya watu wasiopungua 39 katika kipindi cha siku mbili zilizopita.
Mtandao huo wa asasi za kiraia ulikuwa na waangalizi zaidi ya 8,000 waliosambazwa nchini kote kuangalia zoezi la upigaji kura lilivyofanyika siku ya Jumamosi katika uchaguzi ambao Rais Muhammadu Buhari aliwania kuiongoza tena nchi hiyo kwa muhula wa pili.

Kwa mujibu wa kituo hicho kikuu cha asasi za kiraia, tukio baya zaidi la mauaji lilitokea Abonnema katika jimbo la Rivers, lililoko kilomita 14 magharibi mwa mji muhimu zaidi wa sekta ya mafuta wa bandari ya Harcourt ambapo watu saba waliuawa katika ufyatulianaji risasi uliotokea baina ya askari wa serikali na genge lisilojulikana.
Kwa mujibu wa kaimu mkurugenzi wa ofisi ya mahusiano ya umma ya jeshi la Nigeria Kanali Sagir Musa, luteni mmoja wa jeshi na watu sita wenye silaha waliuawa katika mapigano yaliyojiri wakati washambuliaji walipofunga njia kuu ya kuingilia mjini humo na kuwazingira wanajeshi.
Clement Nwankwo, afisa wa kituo cha Situation Room, amesema vifo zaidi ya 260 vilivyotokana na sababu za kisiasa vimetokea nchini Nigeria tangu kampeni za uchaguzi zilipoanza mwezi Oktoba mwaka jana.
Hayo yanaripotiwa katika hali ambayo, mkuu wa ujumbe wa waangalizi wa Umoja wa Afrika ametangaza leo kuwa, uchaguzi wa Nigeria "kwa ujumla ulifanyika katika hali ya amani".../