Shambulizi la anga la Marekani ladaiwa kuua 'magaidi' 35 Somalia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i51805-shambulizi_la_anga_la_marekani_ladaiwa_kuua_'magaidi'_35_somalia
Kamandi ya Jeshi la Marekani barani Afrika (AFRICOM) imedai kuwa mashambulizi ya anga ya wanajeshi wake yamefanikiwa kuangamiza wanachama 35 wa kundi la kigaidi na kitakfiri la al-Shabaab nchini Somalia.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 26, 2019 04:13 UTC
  • Shambulizi la anga la Marekani ladaiwa kuua 'magaidi' 35 Somalia

Kamandi ya Jeshi la Marekani barani Afrika (AFRICOM) imedai kuwa mashambulizi ya anga ya wanajeshi wake yamefanikiwa kuangamiza wanachama 35 wa kundi la kigaidi na kitakfiri la al-Shabaab nchini Somalia.

Marekani inadai kuwa imeshirikiana na jeshi la Somalia katika hujuma hiyo iliyolenga maficho ya wanamgambo hao wa kitakfiri ambao kwa muda mrefu sasa wamekuwa wakipigania kuiangusha serikali ya Mogadishu.

Kwa mujibu wa AFRICOM, hujuma hiyo ya Jumapili ililenga maficho ya al-Shabaab yapata kilomita 37 mashariki mwa mji wa Beledweyne katika eneo la Hiran, katikati mwa nchi karibu na mpaka wa Ethiopia.   

Wanachama wa kundi la ukufurishaji la al-Shabaab

Marekani ilianzisha mashambulizi ya anga yanayofanywa na ndege zake zisizo na rubani 'drone' nchini Somalia mnamo Juni 2011, lakini hujuma hizo zimeshindwa kulitokemeza kundi hilo la ukufurushaji.

Mwishoni mwa mwaka uliopita, utafiti mpya uliofanywa na Taasisi ya Hiraal yenye makao makuu yake mjini Mogadishu ulibainisha kuwa, mashambulizi ya anga yanayofanywa kila uchao na Marekani nchini Somalia yameshindwa kulitokomeza au hata kulidhoofisha kundi hilo  la kigaidi na badala yake yamekuwa na taathira hasi kwa raia wa kawaida.