Burundi yaitaka UN ifunge ofisi zake za haki za binadamu
Burundi imeulazimu Umoja wa Mataifa ufunge ofisi zake za haki za binadamu nchini humo baada ya miaka 23 ya kuendesha shughuli zake katika nchi hiyo ya mashariki mwa Afrika.
Kamishna wa Haki za Binadamu katika Umoja wa Mataifa Michelle Bachelet ametangaza Jumanne kuwa, serikali ya Burundi imesema imepiga hatua za kutosha katika kadhia ya haki za binadamu na hivyo hakuna haja tena ya kuwepo ofisi hiyo ya Umoja wa Mataifa nchini humo.
Bachelet amebainisha masikitiko yake kufuatia hatua hiyo ya Burundi na kusema kuwa ustawi wa haki za binadamu nchini humo ulihatarishwa mwaka 2015 baada ya Rais Pierre Nkurunziza kutangaza kuwania urais kwa muhula wa tatu.
Wataalamu wa haki za binadamu wanasema machafuko yaliyojiri baada ya tangazo hilo yalisababisha ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu. Baada ya Nkurunziza kushinda vikosi vya usalama vilitekeleza oparesheni dhidi ya wapinzani ambapo inadokezwa kuwa mamia walifariki dunia na karibu nusu milioni walikimbilia hifadhi nje ya nchi.
Mnamo Okotaba mwaka 2016, Burundi ilisitisha oparesheni zote za ofisi ya Umoja wa Mataifa nchini humo baada ya ripoti huru ya umoja huo kusema maafisa wa serikali na waungaji mkono wa chama tawala walihusika katika jinai dhidi ya binadamu.
Burundi ilikanusha madia hayo na kumtuhumu Kamishna wa Haki za Binadamu katika Umoja wa Mataifa kuwa alikuwa "anawauza" Waafrika kama iliyovkuwa katika zama za utumwa, tamko ambalo lilimkasirisha sana Bachelet.