Rais wa Somalia: Vita dhidi ya ugaidi nchini haviishi karibuni
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i51970-rais_wa_somalia_vita_dhidi_ya_ugaidi_nchini_haviishi_karibuni
Rais Mohammed Abdullahi Farmajo wa Somalia amekiri kuwa, vita dhidi ya kundi la kigaidi na kitakfiri la al-Shabaab havitamalizika hivi karibuni, lakini akasisitiza kuwa genge hilo limedhoofishwa kwa kiasi kikubwa.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 05, 2019 23:23 UTC
  • Rais wa Somalia: Vita dhidi ya ugaidi nchini haviishi karibuni

Rais Mohammed Abdullahi Farmajo wa Somalia amekiri kuwa, vita dhidi ya kundi la kigaidi na kitakfiri la al-Shabaab havitamalizika hivi karibuni, lakini akasisitiza kuwa genge hilo limedhoofishwa kwa kiasi kikubwa.

Rais Farmajo ameyasema hayo katika mkutano na mawaziri, wakuu wa usalama, wahudumu katika sekta ya matibabu na timu za uoakoaji katika Ikulu ya Mogadishu na kuongeza kuwa, serikali yake itaendelea kusimama kidete katika kupambana na ugaidi.

Amebainisha kuwa, "Ingawa tumelishinda kundi la kigaidi la al-Shabaab katika medani ya vita, lakini kulitokomeza kikamilifu genge hilo sio jambo la kumalizika katika kipindi cha mwaka mmoja au miwili."

Rais wa Somalia amesema jeshi la nchi hiyo kwa kushirikiana na askari wa Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Afrika nchini humo Amisom limepata mafanikio makubwa katika kukabiliana na genge hilo ambalo limepoteza asilimia kubwa ya ngome zake, lakini kibarua cha kulitokomeza kikamilifu kingalipo. 

Wanachama wa kundi la kigaidi la al-Shabaab la Somalia

Itakumbukwa kuwa, Rais Farmajo wa Somalia aliahidi kumaliza uasi wa genge la kigaidi la al-Shabaab katika kipindi cha miaka miwili tu ya uongozi wake, lakini hivi sasa anakabiliwa na changamoto kubwa ya kiusalama kutoka kwa genge hilo.

Mkutano huo wa usalama umefanyika siku chache baada ya magaidi hao wakufurishaji kufanya shambulizi dhidi ya Hoteli ya Makka al-Mukarram mjini Mogadishu, ambapo watu wasiopungua 30 waliuawa.