Magaidi 46 wanaofungamana na Kundi la Daesh waangamizwa Sinai, Misri
(last modified Mon, 11 Mar 2019 16:47:41 GMT )
Mar 11, 2019 16:47 UTC
  • Magaidi 46 wanaofungamana na Kundi la Daesh waangamizwa Sinai, Misri

Jeshi la Misri limeangamiza magaidi 46 wenye mfungamano na kundi la kigaidi la Daesh katika operesheni ya vikosi vya usalama vya nchi hiyo katikati ya mkoa wa Sinai Kaskazini.

Jeshi la Misri limetangaza leo kuwa, makumi ya magaidi wenye mfungamano na kundi la kigaidi la Daesh wameangamizwa katika eneo la Sinai Kaskazini la mashariki mwa nchi hiyo kufuatia operesheni kabambe iliyoendeshwa na vikosi vya usalama vya nchi hiyo.

Taarifa hiyo ambayo haikuashiria ni lini hasa operesheni hiyo ilifanyika, imeeleza kwamba, wanajeshi watatu wa nchi hiyo wameuawa katika mapingano ya hivi karibuni.

Mapigano kati ya askari usalama wa Misri na watu wenye silaha katika mkoa huo wa Sinai Kaskazini ambayo yameua makumi ya raia na maafisa usalama yalishika kasi mwaka 2014 baada ya Rais Abdul Fattah al Sisi kushika madaraka ya nchi hiyo. 

Moja ya vituo vya upekuzi katika mkoa wa Sinai Kaskazini nchini Misri

Takwimu rasmi zinaonyesha kuwa, katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, magaidi 600 wameuawa huko Sinai Kaskazini huku wanausalama 40 wakipoteza maisha yao katika operesheni za kukabiliana na magaidi hao.

Kundi la kigaidi linalojiita Wilaya ya Sinai ambalo ni tawi la kundi la kigaidi na ukufurishaji la Daesh nchini Misri limekuwa likiendesha hujuma katika mkoa huo na limeshauwa makumi ya watu katika operesheni zake dhidi ya raia na askari wa kikosi cha ulinzi cha Misri.