HRW yaitaka ICC ichunguze jinai za kivita nchini Sudan Kusini
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i52130-hrw_yaitaka_icc_ichunguze_jinai_za_kivita_nchini_sudan_kusini
Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limetoa mwito kwa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC kuanzisha uchunguzi wa jinai za kivita nchini Sudan Kusini.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 13, 2019 04:09 UTC
  • HRW yaitaka ICC ichunguze jinai za kivita nchini Sudan Kusini

Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limetoa mwito kwa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC kuanzisha uchunguzi wa jinai za kivita nchini Sudan Kusini.

Taarifa iliyotolewa jana Jumanne na shirika hilo imesema njia pekee ya kumaliza mzunguko wa jinai na mapigano katika nchi hiyo changa zaidi barani Afrika ni kuwawajibisha wahusika wa pande zote, iwe ni wanajeshi wa serikali na waitifaki wao kwa upande mmoja au magenge ya upinzani kwa upande mwingine.

HRW imesema jinai za kivita na dhidi ya binadamu zinaendelea kushuhudiwa katika nchi hiyo barani Afrika, licha ya pande hasimu za kisiasa kusaini makubaliano ya amani mwezi Septemba mwaka uliopita.

Hivi karibuni, shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International liliituhumu serikali ya Sudan Kusini na makundi ya wabeba silaha yanayoungwa mkono na serikali hiyo kwamba yametenda jinai za kivita na ukatili wa kutisha dhidi ya raia.

 

Sudan Kusini ingali inashuhudia mapigano licha ya Kiir na Machar kusaini makubaliano ya amani mara kadhaa

Aidha Kamisheni ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa hivi karibuni ilitoa ripoti kuhusu ukiukwaji wa haki za binadamu na ukatili unaofanyika Sudan Kusini, na kusema kuwa hali hiyo inatia wasiwasi mkubwa.

Sudan Kusini ilijitenga na Sudan mwaka 2011 kwa uchochezi wa nchi za Magharibi hususan Marekani na mwaka 2013 ilitumbukia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe baina ya jeshi la serikali ya Rais Salva Kiir na waungaji mkono wa aliyekuwa makamu wake, Riek Machar.