Waislamu wa Nigeria waandamana tena kushinikiza Sheikh Zakzaky aachiliwe huru
Kwa mara nyingine tena, wananchi Waislamu wa Nigeria wamefanya maandamano ya kutaka kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya nchi hiyo Sheikh Ibrahim Zakzaky aachiliwe huru.
Maandamano hayo yalifanyika jana Jumatano katika mji mkuu wa nchi hiyo Abuja, ambapo waandamanaji wameitaka serikali imwachie huru kiongozi wa harakati ya Kiislamu ya nchi hiyo, Sheikh Zakzaky, ambaye amewekwa kizuizini tokea mwaka 2015.
Kadhalika waandamanaji ambao walikuwa wamebeba mabango ya kumuunga mkono Sheikh Zakzaky, wametaka kuachiwa huru mke wa kiongozi huyo wa Waislamu wa madhehebu ya Kishia nchini Nigeria.
Sheikh Zakzaky alikanusha madai dhidi yake, yakiwemo ya mauaji, kukusanyika kinyume cha sheria, kufanya maandamano pasi na kibali cha vyombo vya usalama miongoni mwa tuhuma nyinginezo.
Sheikh Ibrahim Zakzaky na mkewe walikamatwa na kuwekwa kizuizini tarehe 13 Desemba 2015, wakati askari wa jeshi la Nigeria walipovamia na kufanya hujuma dhidi ya Hussainiyyah ya mji wa Zaria katika jimbo la Kaduna kaskazini mwa nchi hiyo.
Mnamo mwezi Desemba 2016, Mahakama Kuu ya Nigeria ilitoa hukumu ya kutaka Sheikh Zakzaky aachiwe huru mara moja, sambamba na kulitaka jeshi na vyombo vya usalama viilipe familia yake fidia ya dola laki moja na nusu, lakini si tu vimekaidi kutekeleza hukumu hiyo ya mahakama lakini vimeendelea pia kumweka kizuizini kiongozi huyo wa kidini pamoja na mkewe.