Wahajiri haramu zaidi ya 100 watiwa mbaroni nchini Libya
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i52492-wahajiri_haramu_zaidi_ya_100_watiwa_mbaroni_nchini_libya
Kambi moja ya jeshi la Libya imetangaza kuwa wahajiri haramu zaidi ya 100 wametiwa mbaroni katika mji wa Tobruk mashariki mwa nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Mar 30, 2019 02:19 UTC
  • Wahajiri haramu zaidi ya 100 watiwa mbaroni nchini Libya

Kambi moja ya jeshi la Libya imetangaza kuwa wahajiri haramu zaidi ya 100 wametiwa mbaroni katika mji wa Tobruk mashariki mwa nchi hiyo.

Vyombo vya habari vimezinukuu duru za jeshi la Libya zikiripoti kuwa watu 43 miongoni mwa wahajiri hao walikamatwa katika doria iliyofanywa na jeshi kusini mwa mji huo wa Tobruk.

Ripoti hiyo ya jeshi la Libya imeongeza kuwa wahajiiri wengine haramu 60 walitiwa nguvuni katika doria nyingine iliyofanywa na askari wa jeshi hilo.

Kwa mujibu wa Shirika la Kimataifa la Uhajiri IOM, njia ya majini ya kutoka Libya kuelekea nchi za Ulaya ikiwemo Italia na Malta, ndiyo njia hatari zaidi kwa maafa ya roho za watu inayotumiwa na wahajiri haramu kutoka nchi hasa za Kiafrika kwa safari za kuelekea barani Ulaya kwa lengo la kutafuta maisha mazuri.

Mtumbwi unaotumiwa na wahajiri haramu katika safari hatarishi za kuelekea Ulaya ukiwa umezama

Hata hivyo ripoti zinaeleza kuwa asilimia kubwa ya wahajiri hao huwa hawafiki wanakoelekea, bali huishia mikononi mwa magenge ya magendo ya binadamu, kuzama baharini au kupigwa mnada masokoni na kuuzwa kama watumwa.

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) lilitangaza kuwa zaidi ya wahajiri elfu mbili waliaga dunia katika bahari ya Mediterania katika mwaka uliopita wa 2018.../