Mar 30, 2019 07:54 UTC
  • UN: Eritrea imeshindwa kueleza waliko wanasiasa na wanahabari waliotoweka

Wataalamu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa wamesema serikali ya Eritrea imeshindwa kutoa ufafanuzi kuhusu waliko wanaharakati wa kisiasa na waandishi wa habari waliokamatwa na maafisa usalama au waliotoweka katika mazingira ya kutatanisha nchini humo.

Wataalamu 18 wa Kamati ya Haki za Binadamu ya UN wamesema kwamba wamepokea ripoti mbalimbali zinazohusu tuhuma za jinai dhidi ya binadamu ambazo zimekuwa zikifanywa na viongozi na wanasiasa wa nchi hiyo ya Pembe ya Afrika tangu ijipatie uhuru mwaka 1991.

Ripoti ya wataalamu hao imefichua kuwa, mbali na mauaji, ubakaji na ukandamizaji, watawala wa nchi hiyo changa ya Kiafrika wamekuwa wakiwamata au kuwapoteza wanasiasa wakosoaji wake na waandishi wa habari.

Baadhi ya matukio yaliyonakiliwa kwenye ripoti hiyo ya UN, ni kutojulikana hatima ya waandishi wa habari 18 waliokamatwa na maafisa usalama mwaka 2001, mbali na kutoweka katika mazingira ya kutatanisha maafisa 11 wa zamani wa ngazi za juu wa chama tawala, walioandika waraka wa kuikosoa serikali mwaka huo huo.

Ramani ya Eritrea na jirani yake Ethiopia

Wataalamu hao wa masuala ya haki za binadamu wa UN wameashiria pia kitendo cha kutiwa mbaroni aliyekuwa Waziri wa Fedha, Berhane Abrehe na mkewe Almaz Habtemariam mwaka jana, na hadi sasa haijulikani iwapo wapo hai au walishauawa. 

Huko nyuma pia, Umoja wa Mataifa ulitoa wito wa kufikishwa katika Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC viongozi na wanasiasa wa Eritrea, kwa tuhuma za kufanya jinai dhidi ya binadamu.

Tags