Maandamano yaendelea Sudan, polisi wapambana na waandamanaji
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i52627-maandamano_yaendelea_sudan_polisi_wapambana_na_waandamanaji
Polisi ya Sudan imekabiliana na waandamanaji waliokuwa wakiandamana dhidi ya serikali katika mji mkuu wa nchi hiyo Khartoum na maeneo ya kando kando na mji mkuu huo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 04, 2019 10:24 UTC
  • Maandamano yaendelea Sudan, polisi wapambana na waandamanaji

Polisi ya Sudan imekabiliana na waandamanaji waliokuwa wakiandamana dhidi ya serikali katika mji mkuu wa nchi hiyo Khartoum na maeneo ya kando kando na mji mkuu huo.

Taarifa zaidi zinasema kuwa, vyombo vya usalama vya Sudan vimelazimika kutumia mabomu ya gesi ya kutoa machozi kuwatawanya waandamanaji hao katika miji ya Khartoum na Omdurman. Waandamanaji hao walisikika wakipiga nara dhidi ya Rais Omar Hassan al-Bashir na serikali yake.

Aidha waandamanaji hao walikuwa wamebeba mabango na maberamu yenye jumbe mbalimbali zinazotaka kuondoka madarakani Rais Omar Hassan al-Bashir. Taarifa zaidi zinasema kuwa, maandamano kama hayo yameshuhudiwa pia katika miji mingine ya Sudan.

Tangu katikati ya mwezi Desemba mwaka jana hadi sasa, Sudan imekuwa ikishuhudia maandamano makubwa ya kulalamikia hali mbaya ya uchumi na ongezeko la bei za bidhaa.

Rais Omar Hassan al-Bashir

Maandamano ya hivi sasa ya nchini Sudan ni makubwa zaidi kuwahi kuikumba nchi hiyo katika kipindi cha miaka 30 iliyopita. Maandamano hayo yaliyoanza kwa kulalamikia ughali wa maisha yamebadilika na kuwa wimbi la kumtaka Rais Omar al Bashir wa nchi hiyo ang'oke madarakani, lakini bado anashikilia msimamo wake wa kubakia uongozini.

Makumi ya waandamanaji ambao wanataka Rais Omar al-Bashir ang'atuke madarakani wametiwa mbaroni, huku ripoti za asasi za kiraia zikieleza kuwa watu zaidi ya watu 50 wameuawa hadi sasa katika ghasia na machafuko huko Sudan.

Licha ya kutangazwa hali ya hatari na hata kuundwa baraza jipya la mawaziri, yote hayo hayajafanikiwa kutuliza hali ya mambo kwani maandamano hayo yameendelea kushuhudiwa karibu kila siku nchini Sudan.