Watu wengine 5 wauawa katika maandamano ya Sudan
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i52706-watu_wengine_5_wauawa_katika_maandamano_ya_sudan
Kwa akali watu watano wameuawa na maafisa usalama ndani ya masaa 48 yaliyopita, huku maandamano ya kumtaka Rais Omar al Bashir ajiuzulu yakichachamaa nchini Sudan.
(last modified 2026-03-17T04:36:21+00:00 )
Apr 08, 2019 03:27 UTC
  • Watu wengine 5 wauawa katika maandamano ya Sudan

Kwa akali watu watano wameuawa na maafisa usalama ndani ya masaa 48 yaliyopita, huku maandamano ya kumtaka Rais Omar al Bashir ajiuzulu yakichachamaa nchini Sudan.

Sarah Abdel-Jaleel, msemaji wa Jumuiya ya Wataalamu Sudan SPA ameliambia shirika la habari la Associated Press kuwa, watu wanne wameuawa katika maandamano ya mji mkuu Khartoum, huku mmoja akiuawa katika mjini Omdurman siku ya Jumamosi na jana Jumapili.

Nayo Kamati ya Madaktari Sudan ambayo ni mwanachama wa SPA imesema makumi ya watu wamajeruhiwa ndani ya siku mbizi hizo za maandamano katika miji mbalimbali ya Sudan.

Aidha hapo jana nchi nzima ilishuhudiwa kiza kutokana na kukatika umeme, huku serikali ikikosa kutoa maelezo juu ya suala hilo. Waziri wa Nishati amesema wataalamu wao wanashughulikia hitilafu zilizosababisha kukatika umeme nchini humo.

Maelfu ya Wasudan jana kwa siku ya pili mfululizo waliendeleza maandamano yao nje ya nyumba ya Rais Omar al Bashir wa nchi hiyo katika eneo la kati mwa Sudan.

Kwa mujibu wa shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu la Physicians for Human Rights, watu wasiopungua 60 wameuliwa na maafisa usalama nchini Sudan katika kipindi cha miezi mitatu ya ghasia na maandamano dhidi ya utawala wa kiimla wa al-Bashir.

Sudan imekumbwa na maandamano ya kumtaka Rais Omar al-Bashir aachie ngazi tangu katikati ya mwezi Disemba mwaka jana 2018. Chanzo cha maandamano hayo kilikuwa ni kulalamikia kupanda bei za bidhaa muhimu hasa mkate na mafuta.