Jenerali aliyemrithi Omar al-Bashir ajiuzulu pia, maandamano yashtadi Sudan
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i52813-jenerali_aliyemrithi_omar_al_bashir_ajiuzulu_pia_maandamano_yashtadi_sudan
Jenerali Awad Mohamed Ahmad Ibn Auf, Waziri wa Ulinzi wa Sudan aliyetangazwa kuwa Kaimu Rais baada ya Omar al-Bashir kung'olewa madarakani naye ametangaza kujiuzulu, baada ya makumi ya maelfu ya Wasudani kuendeleza maandamano wakitaka makabidhiano ya kiraia ya uongozi.
(last modified 2026-02-05T12:50:29+00:00 )
Apr 13, 2019 04:07 UTC
  • Jenerali aliyemrithi Omar al-Bashir ajiuzulu pia, maandamano yashtadi Sudan

Jenerali Awad Mohamed Ahmad Ibn Auf, Waziri wa Ulinzi wa Sudan aliyetangazwa kuwa Kaimu Rais baada ya Omar al-Bashir kung'olewa madarakani naye ametangaza kujiuzulu, baada ya makumi ya maelfu ya Wasudani kuendeleza maandamano wakitaka makabidhiano ya kiraia ya uongozi.

Jenerali Ibn Auf alitangaza kujiuzulu jana Ijumaa katika hotuba aliyoitoa kupitia televisheni ya taifa, siku moja tu baada ya kuapishwa kuliongoza Baraza la Mpito la Kijeshi lililochukua jukumu la kuiongoza nchi kabla ya uchaguzi kuitishwa.

Katika hotuba hiyo iliyorushwa mubashara jana Ijumaa, askari huyo mkongwe amesema, "Nimefanya uamuzi huu wa kujiuzulu kama Rais wa Baraza la Mpito la Kijeshi kwa maslahi ya taifa. Ningependa mufanye kazi kwa ushirikiano na natumai mtapata suluhisho haraka."

Jenerali Ibn Auf amemteua Luteni Jenerali Abdel Fattah Burhan, Kamanda Mkuu wa Vikosi vya Nchi Kavu kujaza nafasi yake.

Omar Hassan al-Bashir, Rais wa Sudan aliyeachia ngazi kufuatia maandamano ya wananchi

Baada ya kuapishwa juzi, Waziri huyo wa Ulinzi wa Sudan alitangaza kwamba, Baraza la Mpito la Kijeshi litaongoza nchi hiyo kwa muda wa miaka miwili kabla ya kuitishwa uchaguzi mkuu, jambo ambalo liliamsha tena ghadhabu za wananchi waliomiminika mabarabarani kufanya maandamano, licha ya marukufu ya kutoka nje usiku.

Rais Omar Hassan al-Bashir aliyeingia madarakani mwaka 1989 kwa kumpindua kijeshi Sadiq al-Mahdi, ambaye alikuwa Waziri Mkuu wa wakati huo wa Sudan, alipinduliwa na jeshi la nchi hiyo na kuwekwa kizuizini, baada ya kushuhudiwa maandamano ya wananchi ya kumtaka ang'atuke uongozini baada ya miongo mitatu ya utawala wake.