New Zealand, nchi ya kwanza kuikabidhi Rwanda nyaraka za mauaji ya kimbari
New Zealand imekuwa nchi ya kwanza duniani kuikabidhi Rwanda nyaraka zinazohusiana na mauaji ya kimbari ya mwaka 1994.
Baada ya kupokea nyaraka hizo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Rwanda Richard Sezibera amesema, "Katika nchi zote zenye uhusiano wa kihistoria na Rwanda, New Zealand inakuwa ya kwanza kuikabidhi serikali ya Kigali nyaraka ilizokuwa nazo, kuhusiana na mauaji ya kimbari."
Dakta Sezibera amepokea nyaraka hizo za maandishi kutoka kwa Spika wa Bunge la Wawakilishi wa New Zealand , Trevor Mallard.
Haya yanajiri siku chache baada ya Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa kuipatia kamisheni moja ya nchi hiyo jukumu la kufuatilia iwapo Paris ilikuwa na nafasi katika mauaji hayo ya muongo wa 90 nchini Rwanda au la.
Kabla ya hapo pia rais wa zamani wa Ufaransa, François Hollande alijaribu kufichua nyaraka za kihistoria zinazohusiana na jinai hiyo.
Mauaji ya kimbari ya Rwanda yalijiri kwa muda wa siku 100 kuanzia Aprili 6 mwaka 1994 baada ya Rais Juvanal Habyarimana na mwenzake wa Burundi Cyprien Ntaryamira, wote Wahutu, kupoteza maisha wakati ndege yao ilipotunguliwa katika mji mkuu wa Rwanda, Kigali.
Shambulizi hilo lilipelekea wanajeshi wa Kihutu serikali na wanamgambo waitifaki waliokuwa na misimamo mikali kuanzisha mauaji ya kimbari kwa lengo la kuwaangamiza Watutsi waliokuwa wachache. Watutsi 800,000 na Wahutu wenye misimamo ya wastani waliuawa katika mauaji hayo ya kimbari ya Rwanda yaliyojiri miaka 25 iliyopita.