Waandamanaji Sudan kutangaza Baraza la Mpito la Kiraia
Chama cha Wanataaluma Sudan kimetangaza kuwa kinajiandaa kutangaza Baraza la Mpito la Kiraia, litakalochukua madaraka kutokana kwa Baraza la Mpito la Kijeshi la nchi hiyo.
Mohammed al-Asam ambaye ni mwanachama wa ngazi za juu wa baraza hilo la wanataaluma ambalo lilikuwa mstari wa mbele katika kuandaa maandamano dhidi ya utawala wa miaka 30 wa Omar al-Bashir amesema: "Tuko tayari, tuna mpango kabambe wa makabidhiano ya kiraia ya madaraka, na pia tuna majina ya watu waliofuzu kuchukua majukumu hayo."
Hii ni katika hali ambayo, Baraza la Mpito la Kijeshi la Sudan lilitangaza hivi karibuni kuwa litabakia madarakani kwa muda wa miaka miwili ndipo likabidhi madaraka kwa raia, kitendo ambacho kimewakasirisha mno wananchi wa Sudan ambao wanaendelea kufanya maandamano na kukusanyika mbele ya ofisi za jeshi la nchi hiyo mjini Khartoum.
Waandamanaji bado wamekusanyika nje ya Wizara ya Ulinzi mjini Khartoum wakisisitiza kuwa hawataondoka hapo hadi pale raia watakapokabidhiwa madaraka.
Siku chache zilizopita, Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika lililipa baraza hilo la kijeshi la Sudan muda wa siku 15 kuhakikisha linakabidhi madaraka kwa raia, vinginevyo AU itachukua hatua dhidi ya baraza hilo.
Itakumbukwa kuwa, Rais Omar al-Bashir alipinduliwa mnamo Aprili 11 baada ya maandamano ya miezi mitatu ya wananchi; na hivi sasa Baraza la Kijeshi la Mpito chini ya uongozi wa Luteni Jenerali Abdel Fattah al Burhan Abdelrahman limechukua madaraka kwa muda.