Wasudan waendeleza maandamano ya kushinikiza utawala wa kiraia
Maelfu ya wananchi wa Sudan wamesali Sala ya Ijumaa nje ya makao makuu ya jeshi la nchi hiyo mjini Khartoum, siku moja baada ya maandamano makubwa kushuhudiwa katika kona mbalimbali za mji mkuu huo, kulishinikiza jeshi likabidhi madaraka kwa raia.
Waandamanaji hii leo wamesikika wakipiga nara za "Uhuru Uhuru!" wakati ambapo Khatibu wa Sala ya Ijumaa katika eneo hilo, Sheikh Matter Younis akiendelea kutoa hotuba.
Huku hayo yakijiri, muungano wa vyama vya upinzani nchini Sudan unaofahamika kama Uhuru na Mabadiliko umeakhirisha shughuli ya kutangaza wawakilishi wake katika serikali ya kiraia ya nchi hiyo, kutokana na makubaliano yaliyofikiwa kati yake na Baraza la Mpito la Kijeshi katika mkutano wa Jumatano iliyopita.
Baada ya mkutano huo, jeshi lilitangaza kuwa limefikia makubaliano kwa mambo mengi miongoni mwa matakwa ya waandamanaji. Pande hizo mbili ziliafikiana kuunda kamati ya pamoja ili kutatua tofauti zilizopo.
Itakumbukwa kuwa, Rais Omar al-Bashir alipinduliwa mnamo Aprili 11 baada ya maandamano ya miezi kadhaa ya wananchi; na hivi sasa Baraza la Kijeshi la Mpito chini ya uongozi wa Luteni Jenerali Abdel Fattah al Burhan Abdelrahman limechukua madaraka kwa muda.
Hata hivyo wananchi wa Sudan wanalitaka jeshi hilo liharakishe mchakato wa kukabidhi madaraka kwa raia.