UNHCR, SUPKEM zazindua kampeni ya "Ramadhani kwa ajili ya elimu kwa wakimbizi"
Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) kwa ushirikiano na Baraza Kuu la Waislamu nchini Kenya (SUPKEM) limezindua kampeni ya kuwasaidia maelfu ya vijana wakimbizi nchini humo wanaokosa elimu.
Uzinduzi huo umefanyika leo Alkhamisi katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi. Kampeni hiyo ya mwezi mmoja ya kukusanya fedha kwa ajili ya mpango huo itafanyika wakati wa mwezi mtukufu wa Ramadhan unaonza ndani ya siku chache zijazo.
Mwakilishi wa UNHCR nchini Kenya Fat'hia Abdallah amesema kati ya wakimbizi zaidi ya laki nne na 50 elfu wanaoishi nchini Kenya, ni asilimia 13 tu ya watoto wakimbizi waliofikia umri wa kwenda shule wanaosoma.
Amebainisha kuwa, ukosefu wa fedha katika mipango ya elimu ya UNHCR umesababisha ukosefu wa miundombinu na upungufu wa walimu waliohitimu wanaohitajika katika kutoa elimu bora kwa watoto wakimbizi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa SUPKEM Yusuf Nzibo amesema, "Ramadhani ni mwezi mtukufu ambapo Waislamu huelekea katika barabara kujitakasa kiroho na kuongeza kasi ya kuwasaidia wanaokabiliwa na matatizo. Aghalabu ya wakimbizi nchini Kenya wameishi wakihangaika kwa zaidi ya miaka 20. Kwa kutumia kampeni hii, tunaweza kuwaondolea baadhi ya changamoto zinazowakabili."
Haya yanajiri siku chache baada ya serikali ya Kenya kufufua azma yake ya kuifunga kambi ya wakimbizi ya Dadaab kama ilivyokuwa imepanga hapo awali, licha ya aghalabu ya wakimbizi kambini hapo kukataa kujisajili katika mpango wa kurejeshwa kwa khiari katika mataifa walikotoka, ulioanzishwa 2014.
Mnamo 2014, kambi hiyo ilikuwa na wakimbizi zaidi ya 350,000, lakini sasa idadi hiyo imepungua hadi 210,556 ambapo 202,381 wanatoka Somalia. Takwimu za UNHCR zinasema wakimbizi 79,328 kutoka Somalia wamerejea nchini kwao kupitia mpango huo.