Ripoti: Hujuma dhidi ya Misikiti Uholanzi zimeongezeka
-
Hujuma dhidi ya Misikiti Uholanzi zimeongezeka
Ripoti mpya imeonesha kuwa matukio ya vurugu na hujuma dhidi ya misikiti nchini Uholanzi yameongezeka kwa kiwango kikubwa katika kipindi cha muongo mmoja uliopita. Hayo ni kwa mujibu wa utafiti wa mtandao wa misikiti K9.
Takwimu zinaonesha kuwa, jumla ya visa 369 vilirekodiwa kati ya mwaka 2015 hadi 2025, ikilinganishwa na visa 192 katika kipindi cha miaka kumi kilichotangulia. Utafiti huo umetaja matukio ya karibuni katika miji ya The Hague, Waalwijk na Emmeloord, kama ilivyoripotiwa na NL Times Ijumaa.
Mapema mwezi huu mjini Emmeloord, wafanyakazi wa msikiti waligundua mfuko uliokuwa na kurasa zilizochanwa za Qur’ani Tukufu. Imam wa eneo hilo pia aliripoti kupokea simu za vitisho. Ripoti imeeleza kuwa kabla ya tukio hilo, mnyama aliyekufa alikuwa amewekwa karibu na jengo la msikiti.
K9 imesema matukio haya yamekuwa yakiongezeka kwa ukali. Shirika hilo limefafanua kuwa awali visa vilikuwa vimejikita zaidi katika matusi ya maneno, lakini sasa vimegeuka kuwa vitisho vya moja kwa moja na mashambulizi ya kimwili.
K9 ilieleza: “Miaka iliyopita matukio yalikuwa zaidi ya matusi… Sasa kuna vitisho vya kiwango cha juu, ikiwemo wanyama waliokufa, barua za vitisho, na vurugu za kimwili. Kutoka mashambulizi na jaribio la uchomaji moto, hadi mawe kutupwa kupitia madirisha na hata mabomu ya Molotov kurushwa katika misikiti.”
Waislamu nchini Uholanzi ni wachache, wakikadiriwa kuwa takriban asilimia 5 ya idadi ya watu. Ingawa taifa hilo lina historia ya kulinda uhuru wa kidini, mashirika ya misikiti yamekuwa yakiripoti kwa miaka kadhaa wasiwasi kuhusu unyanyasaji, uharibifu wa mali, na athari za kauli za kisiasa katika mitazamo ya umma.