Afisa wa Umoja wa Mataifa: Hali bado ni mbaya huko Gaza
-
Baraza la Usalama la UN
Ramiz Alakbarov, Naibu Mratibu Maalumu wa Umoja wa Mataifa wa Mchakato wa Amani wa Mashariki ya Kati, ameonya kwamba hali katika Ukanda wa Gaza "inaendelea kuwa mbaya," na kusema kuwa familia nyingi haziwezi kumudu kununua kuku na nyama licha ya upatikanaji wa bidhaa za msingi za chakula na kuboreshwa kwa bei za bidhaa hizo.
Alakbarov alisisitiza jana Jumatatu katika mkutano na Baraza la Usalama mjini New York kwamba Umoja wa Mataifa na washirika wake bado wanakabiliwa na changamoto kubwa katika kutoa vifaa vya makazi kama vile mahema na blanketi, akisisitiza haja ya kutafuta suluhisho la haraka la ucheleweshaji huo, wakati majira ya baridi kali yanapokaribia.
Afisa huyo wa Umoja wa Mataifa ameeleza kuwa vurugu zinatishia usitishaji mapigano dhaifu huko Gaza, na amezitaka pande zote kujizuia na kutekeleza majukumu yao chini ya makubaliano ya kusitisha mapigano.
Vilevile ameutaka utawala wa Kizayuni wa Israel kupanua uwezo wa vivuko na kuruhusu kuingizwa vifaa na misaada ya kibinadamu kwa Wapalestina wa Ukanda wa Gaza.
Ramiz Alakbarov pia ameonya kuhusu ongezeko la upanuzi wa vitongoni vya walowezi katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu na kushadidi ukatili dhidi ya Wapalestina, ikiwa ni pamoja na vurugu za walowezi, na kufukuzwa Wapalestina katika makazi yao.
Awali, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA) lilikuwa limetangaza kuwa sera ya Israel ya njaa ya kimuundo katika Ukanda wa Gaza bado inaendelea na kwamba ukosefu mkubwa wa rasilimali za kifedha umesababisha mgogoro wa binadamu katika eneo hilo kwa kiwango kisicho na kifani.