Karibu watu 400 wauawa katika mapigano nchini Libya
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i53263-karibu_watu_400_wauawa_katika_mapigano_nchini_libya
Shirika la Afya Duniani (WHO) limesema kuwa, karibu watu 400 wameshauawa katika mapigano nchini Libya.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
May 04, 2019 08:14 UTC
  • Karibu watu 400 wauawa katika mapigano nchini Libya

Shirika la Afya Duniani (WHO) limesema kuwa, karibu watu 400 wameshauawa katika mapigano nchini Libya.

Shirika hilo limesema kuwa, watu wasiopungua 392 wameshauawa na 936 wengine wameshajeruhiwa tangu tarehe 4 Aprili 2019 wakati Jenerali Khalifa Haftar alipoanzisha mashambulizi ya pande zote dhidi ya mji mkuu wa nchi hiyo Tripoli kwa baraka kamili kutoka kwa madola ajinabi kama Marekani na Saudi Arabia.

Ofisi ya Uratibu wa Masuala ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa imetangaza kuwa, ina wasiwasi sana na idadi kubwa ya wakimbizi wanaokimbia mapigano hayo ambayo hadi hivi sasa yameshapelekea zaidi ya watu 50,000 kukimbia makazi yao.

Maandamano Tripoli, mji mkuu wa Libya

 

Mashirika mbalimbali ya misaada ya kibinadamu yamesema kuwa, sehemu kubwa ya watu wanaokimbia mapigano hayo hukimbilia kwenye nyumba za jamii zao hivyo hakuna takwimu madhubuti inayoweza kuonesha idadi hasa ya wakimbizi hao.

Mapigano katika viunga vya kusini mwa mji mkuu wa Libya, Tripoli  yanaendelea baina ya wapiganaji wa Jenerali Khalifa Haftar na wanajeshi wa serikali ya Umoja wa Kitaifa inayotambuliwa rasmi na jamii ya kimataifa ukiwemo Umoja wa Mataifa.

Kama tulivyosema, Marekani na Saudi Arabia ni miongoni mwa waungaji mkono wakuu wa jenerali muasi, Khalifa Haftar.