Libya: Trump asitishe uungaji mkono wa kigeni kwa Jenerali muasi Haftar
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i53415-libya_trump_asitishe_uungaji_mkono_wa_kigeni_kwa_jenerali_muasi_haftar
Serikali ya Muafaka wa Kitaifa Libya (GNA), ambayo inatambuliwa kimataifa, imemtaka rais Donald Trump wa Marekani asitishe uungaji mkono wa kigeni kwa jenerali muasi Khalifa Haftar ambaye askari wake wanaendeleza hujuma dhidi ya mji mkuu Tripoli.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 11, 2019 08:27 UTC
  • Libya: Trump asitishe uungaji mkono wa kigeni kwa Jenerali  muasi Haftar

Serikali ya Muafaka wa Kitaifa Libya (GNA), ambayo inatambuliwa kimataifa, imemtaka rais Donald Trump wa Marekani asitishe uungaji mkono wa kigeni kwa jenerali muasi Khalifa Haftar ambaye askari wake wanaendeleza hujuma dhidi ya mji mkuu Tripoli.

Haftar ambaye anapata uungaji mkono wa moja kwa moja wa Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), Saudi Arabia na Misri, ametumia wapiganaji wake wanaojiita Jeshi la Kitaifa la Libya katika kuuhujumu mji mkuu wa Libya, Tripoli kwa lengo la kuuteka. Serikali ya Muafaka wa Kitaifa Libya yenye makao yake mjini Tripoli inaongozwa na Waziri Mkuu Fayez al-Serraj.

Katika mahojiano na gazeti la Wall Street Journal Ijumaa, al-Serraj alisema waitifaki wa Marekani wameigeuza Libya kuwa medani ya vita vya niaba na kuonya kuwa hatua hiyo inaweza kuibua wimbi jipya la wakimbizi watakaoelekea Ulaya. Al-Seraj amesema mamia ya Walibya wameuawa tokea Aprili 4 wakati wapiganaji wa Haftar walipoanza kuuhujumu mji wa Tripoli na kuongeza kuwa, zaidi ya Walibya 40,000 wamelazimika kuondoka katika makazi yao huku akionya kuwa yamkini mamia ya maelfu wakakimbilia Ulaya.

Waziri Mkuu wa Serikali ya GNA Libya Fayez al-Serraj

Mwezi uliopita taarifa ya Ikulu ya White House ilisema kuwa, Trump alimpigia simu Haftar na kusema anatambua eti jitihada zake za kupambana na ugaidi na kuvilinda visima vya mafuta ya nchi hiyo.

Ni vyema kuashiria kuwa, Libya ina serikali mbili hasimu, moja ikiwa na makao makuu yake mjini Tobruk, iliyo karibu na Jenerali Haftar, na nyingine ya Umoja wa Kitaifa inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa.

Libya ilitumbukia katika machafuko na vita vya ndani baada ya wanajeshi wa Marekani wakishirikiana na wale wa Shirika la Kijeshi la Nchi za Magharibi (NATO) kuishambulia nchi hiyo na kusaidia harakati za kumuondoa madarakani aliyekuwa kiongozi wa nchi hiyo Muammar Gaddafi hapo mwaka 2011.