Yoweri Museveni ataka viongozi wa "maisha" watawale Afrika, wapinzani wapinga
Rais Yoweri Museveni wa Uganda ameyataka mataifa ya Afrika yaondoe sheria zinazowazuia viongozi wenye umri mkubwa na waiotawala muda mrefu kuwania urais katika nchi zao. Ametoa mwito huo mwezi mmoja baada ya Mahakama ya Juu nchini Uganda kuunga mkono hatua ya bunge la nchi hiyo ya kuondoa ukomo wa kuwania urais nchini humo, ili kumpa nafasi Museveni ya kuendelea kuwa rais.
Rais Museveni amezitaka nchi za Afrika kubadilisha katiba zao na kuongoa vizuzi vinavyowazuia viongozi wenye umri mkubwa na waliotawala muda mrefu kuwania tena urais.
Amesema, ukomo uliowekwa kwenye katiba kama ule wa mihula na ukomo kwenye umri ni vitu ambavyo vinalizuia bara la Afrika kuwa na viongozi wazuri na wenye uzoefu.
Baada ya Mahaka Kuu ya Uganda kuunga mkono Museveni kuendelea kugombea, sasa rais huyo anajiandaa kuwania tena katika uchaguzi wa urais mwaka 2021 na iwapo atatangazwa mshindi, jambo ambalo linatarajiwa na wengi, basi atakuwa mmoja wa viongozi wa Afrika waliotawala muda mrefu zaidi yaani atakuwa ametawala kwa muda wa miaka 40.
Hadi hivi sasa Bunge la Uganda limeshabadilisha katiba mara mbili ili kumpa nafasi Rais Museveni ya kuendelea kuwa rais wa nchi hiyo ya Afrika Mashariki.
Kabla ya kufanyiwa marekebisho, katibu ya Uganda ilikuwa inapiga marufuku mtu aliye na umri wa zaidi ya miaka 75 kugombea tena urais nchini humo.
Hata hivyo kauli hiyo ya Rais Museveni imepingwa na wapinzani wanaosema kuwa ina lengo la kupalilia tawala za kiimla na kidikteta barani Afrika.