Umoja wa Mataifa walaani hujuma kanisani Burkina Faso
Umoja wa Mataifa umelaani vikali shambulio lililofanyika Jumapili kwenye kanisa Katoliki Kaskazini mwa Burkina Faso ambalo limepelekea watu sita wapoteze maisa.
Duru za habari zinasema shambulio hilo lililofanywa na mtu mwenye sialaha lilitokea kwenye mji wa Dablo,ambao umeshuhudia ongezeko la machafuko katika miezi ya karibuni.
Wakati wa shambulio hilo kanisa liliteketezwa kwa moto pamoja na majengo mengine kikiwemo kituo cha afya. Katika ujumbe wake kupitia ukurasa wake wa Twitter Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Maria Espinosa, ametoa wito wa wauaji kuwajibishwa.
Naye Metsi Makhetha, mratibu mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini Burkina Faso, ametoa ujumbe kupitia Twitter yake pia akilaani vikali mashambulizi ya leo Dablo, na kuyaatita ni ya kikatili huku akitoa salamu za rambirambi kwa familia za waathirika na waliopoteza maisha.
Shambulio hilo la risasi limekuja siku chache baada ya tahadhari kutolewa na maafisa wa kibinadamu wa Umoja wa Mastaifa akiwemo Makhetha “kuhusu hali isiyo ya kawaida ya kuongezeka kwa mashambulizi ya silaha Sahel ambayo yanaweka mustakabali wa kizazi chote katika hatari kubwa. “
Machafuko yanasambaa Mali na Niger, lakini pia Burkina Faso na kuna hatari kubwa ya kusambaa katika mataifa mengine ya Afrika Magharibi. Machafuko haya ya karibuni yamesababisha ongezeko la watu wanaotawanywa nchini humo ambapo katika miezi 12 iliyopita kumeshuhudiwa zaidi ya watu 330,000 kukimbia makazi yao mbali na wakimbizi wengine 100,000 katika nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.