Kulaaniwa na Umoja wa Afrika mashambulizi ya watu wenye silaha nchini Ethiopia
Umoja wa Afrika AU umelaani vikali mashambulizi ya watu wenye silaha katika mpaka wa Ethiopia na Sudan Kusini.
Shirika la habari la Xinhua limemnukuu Bi Nkosazana Dlamini Zuma, Mkuu wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika akilaani mashambulio hayo siku ya Ijumaa na kutoa mkono wa pole kwa familia za wahanga hao pamoja na serikali ya Ethiopia. Umoja wa Afrika umeongeza kuwa, uko pamoja na taifa la Ethiopia katika msiba huo. Mkuu huyo wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika aidha amewataka watu wenye silaha wawaachilie huru mara moja watu waliowateka nyara huko Ethiopia. Watu wenye silaha waliotokea Sudan Kusini walilivamia eneo la Gambela la magharibi mwa Ethiopia na kuua watu 208 na kuwajeruhi wengine 75. Aidha waliteka nyara wanawake na watoto wadogo 108. Eneo la Gambela na maeneo ya pambizoni mwake yana zaidi ya wakimbizi 284,000 wa Sudan Kusini ambao wamekimbia machafuko nchini mwao. Huko nyuma pia kulitokea mashambulizi kama hayo kwenye maeneo hayo. Katika mapigano hayo, watu wa kabila la Murle la Sudan Kusini pamoja na wa makabila yanayoishi maeneo ya Upper Nile waliokuwa wamejizatiti kwa silaha za kila namna walivamia ardhi ya Ethiopia na kufanya mauaji ingawa hayakuwa makubwa kama ya mara hii. Licha ya kupita siku kadhaa tangu yatokee mauaji hayo, lakini hadi tunaandika uchambuzi huu wa kisiasa, serikali ya Sudan Kusini ilikuwa imeshindwa kusema chochote kuhusu uvamizi huo. Wakati huo huo Wizara ya Mambo ya Nje ya Ethiopia imesema kuwa, nchi hiyo itaendelea na opereseheni zake za kukabiliana na watu wenye silaha katika mpaka wake na Sudan Kusini. Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Ethiopia amelaani mauaji hayo na kusema kuwa, watu wenye silaha wa kabila ya Murle la Sudan Kusini wamevamia eneo la Gambela karibu na mpaka wa nchi hizo mbili na kufanya mauaji ndani ya ardhi ya Ethiopia kabla ya kurejea tena Sudan Kusini. Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Ethiopia amesema, uchunguzi unandelea ili kubaini iwapo wavamizi hao wana uhusiano na serikali na waasi wa Sudan Kusini au la. Ikumbukwe kuwa Sudan Kusini imetumbukia kwenye mapigano ya ndani tangu mwaka 2013. Raia wengi wa nchi hiyo wamelazimika kukimbilia nchi nyingine ili kusalimisha roho zao. Ni kwa sababu hiyo ndio maana kuna maelefu ya wakimbizi wa Sudan Kusini huko Ethiopia. Ikumbukwe pia kuwa, mwaka jana, Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini alilazimika kukubali kutia saini makubaliano ya amani na waasi ili kukomesha mapigano ya miezi 20 baina ya pande hasimu. Salva Kiir alilazimika kutia saini makubaliano hayo kwa mashinikizo ya kimataifa na kwa kuhofia vikwazo vya Umoja wa Mataifa. Ethiopia ilitoa mchango mkubwa wa kufikiwa makubaliano hayo ambayo pamoja na hayo hadi leo hayajakuwa imara vile inavyotakiwa. Siku ya Jumatatu, Riek Machar, hasimu mkubwa wa Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini alitarajiwa kurejea mjini Juba kwa ajili ya kuunda serikali ya Umoja wa Kitaifa kwa mujibu wa makubaliano hayo, lakini jambo hilo limeakhirishwa. Siku hiyo hiyo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki moon alizungumza kwa simu na Rais Salva Kiir ili kuzipongeza pande hizo mbili kwa makubaliano yao katika mwafaka huo. Wachambuzi wa mambo wanasema kuwa, hali ya kisiasa katika nchi za Sudan Kusini, Ethiopia na nchi nyingine za mashariki mwa Afrika imeathiri vibaya usalama na utulivu wa eneo hilo sambamba na kusababisha mauaji na mashambulio ya mara kwa mara hasa katika maeneo ya mpakani, suala ambalo linazidi kutilia nguvu umuhimu wa kuheshimiwa makubaliano yaliyofikiwa baina ya pande hasimu huko Sudan Kusini.