Jun 15, 2019 12:41 UTC

Maafisa usalama wasiopungua 10 wameripotiwa kuuawa baada ya gari lao kukanyaga bomu la kutegwa ardhini katika kaunti ya Wajir, katika eneo la kaskazini mashariki mwa Kenya.

Mashuhuda wanasema gari hilo aina ya Toyota Landcruiser lililokuwa limebeba maafisa 6 wa Polisi wa Utawala na 5 wa Polisi wa Kawaida liliripuka baada ya kukanyaga bomu hilo, katika barabara ya Khorof Harar-Konton.

Mmoja wa viongozi wa Baraza la Wazee katika eneo hilo, Abdullahi Maalim Riba amewaambia waandishi wa habari kuwa, afisa wa Polisi ya Utawala aliyeponea chupuchupu katika mripuko huo amewataarifu kuwa wenzake wote aliokuwa nao garini wameaga dunia.

Afisa huyo kwa sasa anatibiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Wajir. Baadhi ya duru zingine za habari zimedai kuwa ni maafisa sita tu wa polisi waliouawa katika hujuma hiyo.

Gari la Polisi lililoharibiwa kikamilifu na bomu la kutegwa ardhini

Hapo jana, afisa mmoja wa Polisi ya Akiba aliuawa na mwanachama wa genge la kigaidi na kitakfiri la al-Shabaab katika eneo la Boji Qaras huko huko katika kaunti ya Wajir.

Wanachama wa kundi la kigaidi na kitakfiri la al-Shabaab lenye makao yake nchini Somalia wamekuwa wakijipenyeza nchini Kenya hususan kupitia mipaka ya eneo la Kaskazini Mashariki na kutekeleza mashambulizi ya kutisha dhidi ya raia na maafisa usalama. 

Tags