Al-Shabaab: Tumehusika na mashambulizi ya Kenya na Somalia yaliyoua 16
Kundi la kigaidi na kitakfiri la al-Shabaab limetangaza kuwa limehusika na miripuko ya mabomu iliyoua watu 16 hapo jana Jumamosi katika nchi za Kenya na Somalia.
Msemaji wa Operesheni za Kijeshi wa al-Shabaab, Abdiasis Abu Musab, amesema genge hilo la ukufurishaji ndilo lililotekeleza mashambulizi ya mabomu jana huko Kaskazini Mashariki mwa Kenya na katika mji mkuu wa Somalia, Mogadishu.
Abdikadir Abdirahman, Mkurugenzi wa Shirika la Ambulensi la Aamin nchini Somalia amesema miripuko miwili ilishuhudiwa jana mjini Mogadishu karibu na makutano ya barabara ya K4, ambapo wa kwanza uliua watu wanane na kujeruhiwa wengine 16, lakini wa pili ulitibuliwa na maafisa usalama.
Nchini Kenya mashuhuda wanasema gari la polisi aina ya Toyota Landcruiser lililokuwa limebeba maafisa 6 wa Polisi wa Utawala na 5 wa Polisi wa Kawaida liliripuka baada ya kukanyaga bomu la kutegwa ardhini, katika barabara ya Khorof Harar-Konton, katika kaunti ya Wajir, katika eneo la kaskazini mashariki mwa nchi, ambapo askari wanane waliaga dunia.
Hata hivyo afisa wa Polisi ya Utawala aliyeponea chupuchupu katika mripuko huo amewataarifu mashuhuda kuwa wenzake wote 10 aliokuwa nao garini wameaga dunia.
Wanachama wa kundi la kigaidi na kitakfiri la al-Shabaab lenye makao yake nchini Somalia mbali na kutekeleza hujuma na ukatili wa kila namna katika nchi hiyo ya Pembe ya Afrika, lakini pia wamekuwa wakijipenyeza nchini Kenya hususan kupitia mipaka ya eneo la Kaskazini Mashariki na kutekeleza mashambulizi ya kutisha dhidi ya raia na maafisa usalama.