Fayez al-Sarraj ataka uchaguzi ufanyike Libya kabla ya kumalizika mwaka
Waziri Mkuu wa serikali ya umoja wa kitaifa ya Libya ametoa mwito wa kufanyika uchaguzi nchini humo kabla ya mwisho wa mwaka huu. Awali uchaguzi mkuu nchini humo ulikuwa umepangwa kufanyika Disemba 10 mwaka jana 2018 lakini zoezi hilo liliahirishwa kutokana mpasuko uliojitokeza baina ya viongozi wa mirengo hasimu ya kisiasa na wimbi la mapigano na machafuko yaliyozuka katika mji mkuu wa nchi hiyo, Tripoli.
Fayez al Sarraj amesema hayo katika kikao na waandishi wa habari mjini Tripoli na kusisitiza kuwa, kufanyika uchaguzi wa rais na bunge kabla ya kumalizika mwaka huu kutahitimisha mgogoro wa ndani unaoshuhudiwa nchini humo.
Amebainisha kuwa, bado kuna fursa ya kusitisha mapigano na kurejea kwenye meza ya mazungumzo makundi mbalimbali ya ndani ya nchi hiyo. Ametoa mwito wa kuundwa 'Jukwaa la Libya' ambalo litatumika kujadili njia za kuupatia ufumbuzi mgogoro wa nchi hiyo, sambamba na kuandaa ramani ya njia na mazingira ya kufanyika uchaguzi huo.
Waziri Mkuu wa serikali ya umoja wa kitaifa ya Libya kwa mara nyingine tena amebainisha kuwa fursa bado ipo ya kusitisha umwagaji damu na kurejea kwenye meza ya mazungumzo.
Mwito huo wa Sarraj umetolewa katika hali ambayo, kundi linalojiita jeshi la kitaifa la Libya ambalo kwa miaka kadhaa sasa linaungwa mkono na Saudi Arabia, Misri, Imarati na baadhi ya nchi za magharibi linaendelea kumwaga damu za raia, katika vita vyake vya kutaka kudhibiti mji mkuu Tripoli.
Itakumbukwa kuwa, mkutano wa kujadili mgogoro wa Libya na maandalizi ya uchaguzi ujao nchini humo uliotazamiwa kufanyika kati ya Aprili 14 na 16 magharibi mwa nchi hiyo yenye utajiri wa mafuta uliakhirishwa kutokana na kushadidi mapigano yaliyoanzishwa na Haftar Aprili 4 dhidi ya vikosi vya jeshi la Serikali ya Maafikiano ya Kitaifa mjini Tripoli.