Mgombea wa chama tawala ajitangaza mshindi wa uchaguzi wa rais Mauritania
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i54303-mgombea_wa_chama_tawala_ajitangaza_mshindi_wa_uchaguzi_wa_rais_mauritania
Mgombea urais wa chama tawala nchini Mauritania Mohammad Ould Ghazouani amejitangaza mshindi katika uchaguzi huo uliofanyika jana.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 23, 2019 09:11 UTC
  • Mgombea wa chama tawala ajitangaza mshindi wa uchaguzi wa rais Mauritania

Mgombea urais wa chama tawala nchini Mauritania Mohammad Ould Ghazouani amejitangaza mshindi katika uchaguzi huo uliofanyika jana.

Ghazouani, ambaye aliwahi kuwa waziri wa ulinzi, amejitangaza mshindi mapema Jumapili akiwa ameandamana na rais wa sasa Mohamed Ould Abdel Aziz.

Duru katika Tume Huru ya Uchaguzi ya Mauritani (CENI) zimedokeza kuwa Ghazouani alikuwa amepata asilimia 50.56 ya kura zote zilizopigwa baada ya asilimia 80 ya kura kuhesabiwa.

Ghazouani amewaambia wafuasi wake kuwa kura zilizosalia haziwezi kubadilisha matokeo ya mwisho ambayo yanaashiria ushindi wake.

Duru za CENI zimedokeza kuwa  wagombea wa upinzani, Sidi Mohamed Ould Boubacar, waziri mkuu wa zamani, na  Biram Ould Dah Ould Abeid walikuwa wamepata asilimia 18 ya kura kila mmoja wakati zoezi la kuhesabu kura likiendelea.

Wawili hao walikuwa wamelalamika kuwa kulikuwa na dosari katika zoezi la kupiga kura na kwamba wawakilishi wao walitimuliwa kutoka baadhi ya vituo vya kupigia kura. Hata hivyo CENI imesema hakuna matatizo makubwa yaliyoripotiwa katika upigaji kura.

Rais anayeondoka wa Mauritania Ould Abdel Aziz

Rais anayeondoka Ould Abdel Aziz, mwenye umri wa miaka 62 aliingia madarakani kupitia mapinduzi ya kijeshi mwaka 2008 na kushinda chaguzi mbili za 2009 na 2014.

Uchaguzi wa Jumapili ukikamilika kwa mafanikio, utapelekea Mauritania kushuhudua ukabidhianaji madaraka kwa amani kwa mara ya kwanza tokea nchi hiyo ijinyakulie uhuru kutoka Ufaransa mwaka 1960. Wapinzai hata hivyo wamebainisha wasiwasi wao kuhusu idadi kubwa ya wanajeshi wanaohudumua katika serikali ya nchi hiyo.