Aliyepanga mapinduzi yaliyofeli Ethiopia auawa, 182 wakamatwa
Mkuu wa usalama katika jimbo la Amhara, kaskazini mwa Ethiopia anayetuhumiwa kupanga jaribio la kuipindua serikali ya jimbo hilo ameuawa.
Nigussu Tilahun, msemaji wa Ofisi ya Waziri Mkuu wa Ethiopia amesema Brigedia Jenerali Asamnew Tsige aliuawa jana Jumatatu katika makabiliano na maafisa usalama katika mji wa Bahir Dar, viungani mwa makao makuu ya jimbo hilo.
Amesema watu 182 wanaotuhumiwa kuwa wapiganaji watiifu na wafuasi wa mkuu huyo wa usalama katika jimbo la Amhara wametiwa mbaroni katika msako mkali wa jana Jumatatu.
Huku hayo yakiarifiwa, Mwanasheria Mkuu wa eneo hilo ameaga dunia kutokana na majeraha ya risasi aliyoyapata wakati wa ghasia na machafuko ya jaribio hilo la mapinduzi lililofeli.
Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed alihutubia taifa siku chache zilizopita kuhusu kufeli kwa jaribio hilo la mapunduzi dhidi ya serikali ya jimbo la Amhara, lakini alithibitisha habari ya kuuawa Mkuu wa Jeshi la Ethiopia, Jenerali Seare Mekonnen, Rais wa Jimbo la Amhara, Ambachew Mekonnen miongoni mwa maafisa wengine wa ngazi za juu serikalini katika jaribio hilo la mapinduzi ambalo lilitekelezwa na wapiganaji wa Brigedia Jenerali Asamnew Tsige.
Siku chache kabla ya mapinduzi hayo yaliyofeli, Jenerali Asamnew aliwatangazia wazi watu wa kabila la Amhara, moja ya makabila makubwa zaidi nchini Ethiopia kujizatiti kwa silaha, hatua ambayo ilizusha wasiwasi katika nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.