Baada ya kupata pigo, hatimaye Jenerali Khalifa Haftar alazimika kukubali mazungumzo Libya
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i54397-baada_ya_kupata_pigo_hatimaye_jenerali_khalifa_haftar_alazimika_kukubali_mazungumzo_libya
Wapiganaji wanaojiita Jeshi la Taifa la Libya wamelazimika kukubali mazungumzo ya kuutafutia ufumbuzi mgogoro wa nchi hiyo ulioanzishwa na kundi hilo linaloungwa mkono na Saudi Arabia, Imarati, Misri na Ufaransa.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 27, 2019 06:35 UTC
  • Baada ya kupata pigo, hatimaye Jenerali Khalifa Haftar alazimika kukubali mazungumzo Libya

Wapiganaji wanaojiita Jeshi la Taifa la Libya wamelazimika kukubali mazungumzo ya kuutafutia ufumbuzi mgogoro wa nchi hiyo ulioanzishwa na kundi hilo linaloungwa mkono na Saudi Arabia, Imarati, Misri na Ufaransa.

Televisheni ya "Rusia al Yaum" imemnukuu Ahmed al Mesmari, msemaji wa "Jeshi la Taifa la Libya" linaloongozwa na jenerali muasi Khalifa Haftar, akisema leo Alkhamisi mbele ya waandishi wa habari kuwa, wako tayari kushiriki katika mazungumzo lakini wasiwemo watu waliotenda jinai nchini Libya. 

Ulegezaji kamba huo wa "Jeshi la Taifa la Libya" umekuja huku kukiwa na taarifa kwamba jeshi la serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Libya imekomboa sehemu muhimu za kusini mwa Tripoli, mji mkuu wa nchi hiyo kutoka mikononi mwa wapiganaji wa Khalifa Haftar.

Jenerali muasi Khalifa Haftar katika mazungumzo na mfalme wa Saudi Arabia

 

Jenerali huyo muasi amebadilisha msimamo katika hali ambayo katikati ya mwezi huu wa Juni, Aguila Saleh, Spika wa Bunge la Tobruk linalomuunga mkono Khalifa Haftar huko Libya alisema kuwa hawatoshiriki katika mazungumzo yoyote ya amani hadi pale watakapoipindua serikali ya Umoja wa Kitaifa na kuiteka Tripoli, mji mkuu wa nchi hiyo.

Jana Jumatano, jeshi la Serikali ya Umoja wa Kitaifa inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa ilifanikiwa kuukomboa mji wa Garyan wa kusini magharibi mwa Libya uliokuwa umetekwa na wapiganaji wa Khalifa Haftar. Mji huo ulikuwa muhimu sana kwa jenerali muasi Khalifa Haftar na ndicho kilichokuwa kituo kikuu cha kupanga na kuendeshea operesheni za kijeshi dhidi ya Tripoli. 

Nchi ya Libya yenye utajiri mkubwa wa mafuta inaongozwa na serikali mbili hasimu, moja yenye bunge lake huko Tobruk na nyingine ya Tripoli inayotambuliwa na jamii ya kimataifa ukiwemo Umoja wa Mataifa.