Askari wa Ufaransa na Imarati wanaswa wakishirikiana na Haftar, Libya
-
Makamanda wa Haftar waliokamatwa na askari wa Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa
Askari wa Ufaransa na Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) wamekuwa wakishirikiana na wapiganaji wa kundi la Jenerali Khalifa Haftar linalopiganaji dhidi ya serikali inayotambuliwa rasmi kimataifa ya Libya.
Televisheni ya al Jazeera imeripoti kuwa, kamanda Ali muhammad al Sheikhi wa chumba cha operesheni za vita cha kundi linalojiita Jeshi la Taifa chini ya uongozi wa mbabe wa vita, Jenerali Khalifa Haftar katika mji wa Gharyan huko kusini mwa jiji la Tripoli, amefichua kwamba, askari wa Ufaransa na Imarati wamekuwa wakishiriki katika vikao vya chumba cha operesheni za kivita katika mji huo kwa shabaha ya kuuteka mji wa Tripoli.
Vilevile picha zilizosambazwa na baadhi ya watumiaji wa mitandao ya kijamii zinawaonesha mamluki wa Kiafrika wakiwemo wanajeshi wa Wasudani wakipigana bega kwa bega na wapiganaji wa Jenerali Khalifa Haftar na baadhi yao wametekwa nyara na jeshi la Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa.
Jumatano iliyopita jeshi hilo lilikomboa mji wa Gharyan kutoka mikononi mwa wapiganaji wa Khalifa Haftar na kulidhibiti eneo hilo muhimu. Mji huo ulikuwa ukitumiwa kama makao makuu ya wapiganaji wa Haftar katika operesheni ya kutaka kuuteka mji mkuu wa Libya, Tripoli.
Jeshi la Haftar lilianza mashambulizi makali dhidi ya mji wa Tripoli tarehe 4 Aprili likisaidiwa na Saudi Arabia, Misri, Imarati na baadhi ya nchi za Magharibi lakini mpango wa kuteka mji huo umezimwa na kufeli.