Makombora ya Marekani yanaswa Libya katika ngome ya Haftar
Wanajeshi wa serikali ya Umoja wa Kitaifa inayoongozwa na Waziri Mkuu Fayez al-Sarraj na ambayo inaungwa mkono na jamii ya kimataifa wamenasa makombora ya Marekani yaliyokuwa yakitumiwa na vikosi vinavyojiita Jeshi la Kitaifa linaloongozwa na kamanda muasi Khalifa Haftar.
Jana Jumamosi jeshi la serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Libya liliwaonyesha waandishi wa habari mjini Tripoli makombora hayo aina ya Javelin yaliyotengenezewa Marekani, na yaliyokuwa yakitumiwa na wapiganaji wa jenerali muasi Khalifa Haftar.
Silaha hizo zimepatikana katika mji wa Gharyan, kusini mwa mji mkuu Tripoli. Baadhi ya duru za habari zimedai kuwa, maroketi ya China yamepatikana pia katika mji huo wa kistratajia.
Jumatano iliyopita jeshi hilo la serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Libya lilikomboa mji huo wa Gharyan kutoka mikononi mwa wapiganaji wa Khalifa Haftar na kulidhibiti eneo hilo muhimu, lililokuwa likitumiwa kama makao makuu ya wapiganaji wa Haftar katika operesheni ya kutaka kuuteka mji mkuu wa Libya, Tripoli.
Haya yanajiri siku chache baada ya televisheni ya al Jazeera ya Qatar kufichua kuwa, askari wa Ufaransa na Imarati wamekuwa wakishiriki katika vikao vya chumba cha operesheni za kivita katika mji huo kwa shabaha ya kuuteka mji wa Tripoli.
Jeshi la Haftar lilianzisha mashambulizi makali dhidi ya mji wa Tripoli tarehe 4 Aprili likisaidiwa na Saudi Arabia, Misri, Imarati na baadhi ya nchi za Magharibi lakini mpango wa kuteka mji huo umezimwa na kufeli.