Seneti yataka kuchunguzwa uwepo wa silaha za Marekani nchini Libya
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i54530-seneti_yataka_kuchunguzwa_uwepo_wa_silaha_za_marekani_nchini_libya
Mkuu wa Kamati ya Baraza la Seneti la Marekani ametoa wito wa kufanyika uchunguzi kuhusu silaha za nchi hiyo zilizotumiwa na jeshi la jenerali muasi wa Libya Khalifa Haftar.
(last modified 2026-01-14T08:12:18+00:00 )
Jul 03, 2019 08:23 UTC
  • Seneti yataka kuchunguzwa uwepo wa silaha za Marekani nchini Libya

Mkuu wa Kamati ya Baraza la Seneti la Marekani ametoa wito wa kufanyika uchunguzi kuhusu silaha za nchi hiyo zilizotumiwa na jeshi la jenerali muasi wa Libya Khalifa Haftar.

Bob Menendez amesema kuwa, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Mike Pompeo anapaswa kuanzisha uchunguzi kuhusu faili hili. 

Seneta huyo wa jimbo la New Jersey amesema kuwa Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) umekuwa na nafasi kubwa katika kulipatia jeshi la Khalifa Haftar makombora ya Kimarekani ya Javelin na kuongeza kuwa, hatua hiyo inakiuka sheria.

Bob Menendez amesema kuwa, iwapo ripoti zilizotolewa kuhusiana na suala hilo zitakuwa za kweli serikali ya Donald Trump italazimika kutekeleza sheria na kusitisha uuzaji silaha kwa serikali ya Imarati.

Makumi ya raia wameuawa Libya katika mashambulizi ya Khalifa Haftar

Msemaji wa Jeshi la Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa ya Libya Kanali Mohammed Gununu Jumamosi iliyopita aliituhumu Imarati kuwa inaingilia masuala ya ndani ya Libya na inampatia misaada ya kijeshi Jenerali Khalifa Haftar. Alisema kuwa baada ya jeshi la Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa ya Libya kukomboa mji wa kistratijia wa Gharyan kutoka kwa wapiganaji wa Haftar, kumegunduliwa salaha za kisasa za Marekani ambazo zilikuwa kwenye maboksi yenye jina la Imarati. 

Itakumbukwa pia kwamba, zaidi ya wahajiri 40 waliuawa na makumi ya wengine kujeruhiwa katika shambulizi lililofanywa wanamgambo waitifaki wa vikosi vya Khalifa Haftar jana jioni katika mji wa Tajoura, viungani mwa Tripoli.