AU yalaani kushambuliwa wahajiri nchini Libya
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i54534-au_yalaani_kushambuliwa_wahajiri_nchini_libya
Mkuu wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika amelaani shambulio la anga lililofanywa na jenerali muasi Khalifa Haftar dhidi ya kituo cha kuhifadhia wahajiri karibu na Tripoli, mji kuu wa Libya.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jul 04, 2019 02:43 UTC
  • AU yalaani kushambuliwa wahajiri nchini Libya

Mkuu wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika amelaani shambulio la anga lililofanywa na jenerali muasi Khalifa Haftar dhidi ya kituo cha kuhifadhia wahajiri karibu na Tripoli, mji kuu wa Libya.

Moussa Faki Mahamat amesema katika taarifa yake ya jana Jumatano kwamba Umoja wa Afrika unalaani vikali shambulizi la anga dhidi ya kituo cha kuhifadhia wahajiri karibu na mji mkuu wa Libya  na unataka uchunguzi huru ufanyike kuhusu shambulio hilo.

Taarifa hiyo imehimiza kuchukuliwa hatua kali wahusika wote wa mauaji hayo ya kutisha dhidi ya raia na wakati huo huo imetaka kusimamishwa vita mara moja nchini Libya. Kwa upande wake, mjumbe maalumu wa Umja wa Mataifa katika masuala ya Libya, Ghassan Salamé, amelaani vikali kushambuliwa kituo hicho cha kuhifadhi wahamiaji karibu na Tripoli.

Moussa Faki Mahamat

 

Mapema jana asubuhi, ndege za wanamgambo wanaojiita "Jeshi la Taifa la Libwa" wakiongozwa na jenerali muasi Khalifa haftar zilishambulia kituo cha kuhifadhia wahajiri walioingia kinyemela nchini Libya, karibu na mji mkuu Tripoli na kuua wahamiaji 40 na kujeruhi wengine 80.

Jenerali Khalifa Haftar anaungwa mkono na Saudi Arabia, Misri, Imarati na Ufaransa na anashikilia maeneo ya mashariki mwa Libya. Tangu tarehe 4 Aprili mwaka huu na baada ya kutembelea Saudi Arabia, Jenerali Khalifa Haftar alitoa amri ya kushabuliwa mji mkuu wa Libya, Tripoli. Mashambulio hayo yalikuja muda mchache baada ya rais wa Marekani, Donald Trump kuzungumza kwa simu na jenerali huyo muasi na kumuunga mkono katika kile alichodai ni kuendesha vita dhidi ya ugaidi na kulinda usalama wa visima vya mafuta. Zaidi ya watu 740 wameshauwa na wasiopungua 4400 wameshajeruhiwa huko Tripoli tangu wakati huo.