14 wauawa katika mapigano Tripoli, mji mkuu wa Libya
Maafisa jeshi wa Libya wamearifu kuwa watu 14 wameuawa katika mapigano huko Tripoli mji mkuu wa nchi hiyo.
Wameripoti kuwa watu 14 wameuawa katika mapigano kati ya askari jeshi wa serikali ya umoja wa kitaifa na wanamgambo wanaojiita jeshi la kitaifa la Libya wenye mfungamano na kamanda Khalifa Haftar. Wanamgambo hao chini ya uongozi wa Jenerali Khalifa Haftar wamesema kuwa wamefanikiwa kuzuia shambulio la askari wa serikali ya umoja wa kitaifa kusini mwa mji mkuu Tripoli.
Askari jeshi wenye mfungamano na serikali ya umoja wa kitaifa ya Libya walianzisha shambulio hilo leo asubuhi na kuzuiwa na wanamgambo wa jeshi la kitaifa la Libya. Kundi hilo linalojiiita jeshi la kitaifa la Libya ambalo kwa miaka kadhaa sasa linayashikilia maeneo ya mashariki mwa Libya kwa uungaji mkono wa Saudia, Misri, Imarati na baadhi ya nchi za Magharibi lilianzisha mashambulizi tangu Aprili nne mwaka huu kwa lengo la kuuteka mji mkuu Tripoli. Watu zaidi ya elfu moja wameuawa na wengine wasiopungua 4,400 kujeruhiwa tangu kuanza mashambulio hayo hadi sasa.