UNHCR: Mapigano Libya yamefanya watu 120,000 wakimbie makazi yao
Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR limesema watu zaidi ya 120,000 wamelazimika kuwa wakimbizi wa ndani kutokana na mapigano huko Tripoli mji mkuu wa Libya na viunga vyake.
Taarifa ya UNHCR imesema mapigano hayo kati ya askari jeshi wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa inayoungwa mkono na jamii ya kimataifa na wanamgambo wanaojiita Jeshi la Kitaifa la Libya wenye mfungamano na kamanda Khalifa Haftar yamepelekea watu 120,000 kukimbia nyumba zao mjini Tripoli na kutorokea katika miji na maeneo mengine ya nchi.
Kwa mujibu wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa, mapigano yamesababisha asilimia kubwa ya majengo kuporomoka na miundombinu kuharibiwa kikamilifu katika wilaya ya Al-Sabri Al-Sharqi mjini Benghazi.
Kwa uungaji mkono wa Saudi Arabia, Imarati na Ufaransa, vikosi vya mashariki mwa Libya vinavyojiita Jeshi la Taifa, ambavyo vinaongozwa na jenerali muasi Khalifa Haftar, mnamo tarehe 4 Aprili vilianzisha mashambulio dhidi ya mji mkuu wa Libya, Tripoli lakini havijafanikiwa kuudhibiti mji huo.
Kwa mujibu wa takwimu mpya za Shirika la Afya Duniani WHO, watu zaidi ya elfu moja wameuawa na wengine wasiopungua 5,700 wamejeruhiwa tangu yaanze mashambulio hayo hadi sasa.
Kundi hilo linalojiiita Jeshi la Kitaifa la Libya kwa miaka kadhaa sasa linayashikilia maeneo ya mashariki mwa Libya.