Misri yarefusha muda wa hali ya hatari kwa miezi 3 mingine
(last modified Mon, 22 Jul 2019 06:59:45 GMT )
Jul 22, 2019 06:59 UTC
  • Misri yarefusha muda wa hali ya hatari kwa miezi 3 mingine

Rais Abdul-Fattah al-Sisi wa Misri ametangaza kuongeza muda wa hali ya hatari nchini humo kwa kipindi cha miezi mitatu mingine.

Kwa mujibu wa agizo la Rais Abdul-Fattah al-Sisi, amri hiyo ya hali ya hatari itaanza kutekelezwa Alkhamisi ijayo.

Kwa mara ya kwanza Misri ilianza kutekeleza hali ya hatari nchini mwezi Aprili mwaka 2017 baada ya kutokea milipuko katika makanisa mawili na kuuawa watu wasiopungua 45.

Hali ya hatari nchini Misri imeongezewa muda wake kwa amri ya Rais Abdul-Fattah al-Sisi katika hali ambayo umepita mwezi mmoja tangu Muhammad Mursi Rais wa zamani wa nchi hiyo afariki dunia.

Hali hii ya hatari inatoa mwanya kwa askari usalama kuchukua hatua zinazohitajika kukabiliana na hatari, ufadhili kwa makundi ya kigaidi na pia kudhamini usalama katika maeneo yote ya nchi.

Rais Abdul-Fattah al-Sisi

Hali ya hatari nchini Misri inawapatia maafisa husika madaraka makubwa ya kuwatia mbaroni na kuwadhibiti wale wanaotajwa kuwa ni maadui wa nchi.  Vikosi vya usalama vya Misri vimekuwa vikipambana na oparesheni za wanamgambo magaidi wenye ngome zao katika eneo la Sinai ya kaskazini. Mwezi Februari mwaka jana jeshi la Misri lilianzisha operesheni kubwa ya kuwasaka wanamgambo hao magaidi.

Serikali yay Rais al-Sisi inalaumiwa na asasi mbalimbali za haki za binadamu kwamba, imekuwa ikitumia mkono wa chuma kuwakandamiza wapinzani wa nchi hiyo.

Tags