Waislamu 6 wafuasi wa Sheikh Zakzaky wauawa kwa kupigwa risasi, Abuja
Wafuasi 6 wa kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria wameuawa kwa kupigwa risasi na polisi wa Nigeria mjini Abuja.
Shirika la habari la Ufaransa limeripoti kuwa, watu hao sita wameuawa wakati wafuasi wa Sheikh Ibrahim Zakzaky walipokuwa katika maandamano ya amani katika mji mkuu wa Nigeria, Abuja.
Watu walioshuhudia na mwandishi habari wa shirika la habari la Ufaransa wanasema, waandamanaji wasiopungua sita wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria wameuawa kwa kupigwa risasi na polisi.
Abdullah Muhammad Belo ambaye ni miongoni mwa viongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria amesema kuwa, wafuasi wa harakati hiyo walikuwa katika maandamano ya amani na walipofika karibu na jengo la Wizara ya Mambo ya Nje walishambuliwa na jeshi la polisi ambalo liliwafyatulia risasi waandamanaji hao na kuua sita miongoni mwao.
Mwaka 2015, jeshi la Nigeria lilivamia na kushambulia mkusanyiko wa Waislamu katika Husseiniya ya Zaria kwenye jimbo la Kano na kuua shahidi kwa umati karibu Waislamu elfu moja akiwemo watoto watatu wa Sheikh Ibrahim Zakzaky.
Sheikh Zakzaky mwenyewe na mkewe pia walipigwa risasi na tangu wakati huo wanashikiliwa katika korokoro za serikali ya Rais Muhammadu Buhari ambayo inaendelea kukaidi amri ya Mahakama Kuu ya kumwachilia huru mwanachuoni huyo.
Ripoti mbalimbali za kuaminika zinasema kuwa hali ya kiafya ya Sheikh Ibrahim Zakzaky ni mbaya na hata damu yake imegunduliwa kuwa na chembe chembe za risasi kutokana na mateso anayopewa huku hali yake na mkewe ikizidi kuwa mbaya, siku baada ya siku.