Mapigano yashtadi kusini mwa Tripoli mji mkuu wa Libya
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i54985-mapigano_yashtadi_kusini_mwa_tripoli_mji_mkuu_wa_libya
Mapigano kati ya wanamgambo kwa jina la jeshi la kitaifa la Libya na vikosi vya serikali ya umoja wa kitaifa ya Libya yamepamba moto katika eneo la al Ramla kusini mwa Tripoli mji mkuu wa nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 25, 2019 06:46 UTC
  • Mapigano yashtadi kusini mwa Tripoli mji mkuu wa Libya

Mapigano kati ya wanamgambo kwa jina la jeshi la kitaifa la Libya na vikosi vya serikali ya umoja wa kitaifa ya Libya yamepamba moto katika eneo la al Ramla kusini mwa Tripoli mji mkuu wa nchi hiyo.

Mapigano hayo ambayo pande mbili zinatumia silaha nzito yameripotiwa kuanza tangu jana usiku katika eneo la al Amra na huko Ain Zara karibu na uwanja wa ndege wa Tripoli; na hakuna upande wowote uliotoa pigo kwa upande wa pili. Kamanda Khalifa Haftar kiongozi wa wanamgambo hao wanaojiita jeshi la kitaifa la Libya amedai kuwa wapiganaji wake wanakaribia kupata ushindi na kuwataka wajiandae kusonga mbele kuelekea katika mji mkuu Tripoli. 

Baraza Kuu la Uongozi la Libya wiki iliyopita lilitahadharisha kuhusu shambulio tarajiwa la wanamgambo hao wanaoongozwa na Khalifa Haftar na kueleza kuwa Misri, Imarati na Ufaransa zinaunga mkono shambulio hilo. Hali ya mambo imepamba moto huko Libya tangu Aprili nne mwaka huu baada ya Khalifa Haftar kuwaamuru wapiganaji wake waushambulie mji mkuu wa Libya, Tripoli. 

Kamanda Khalifa Haftar, Kiongozi wa wanamgambo wa jeshi la kitaifa la Libya 
 

Wanamgambo hao watiifu kwa Khalifa Haftar wanaoungwa mkono na Imarati, Saudia na Ufaransa wanadhibiti eneo la mashariki mwa Libya huku jeshi la kitaifa la Libya linaloongozwa na Waziri Mkuu Fayez al Siraj likiungwa mkono na jamii ya kimataifa. Jeshi hilo linadhibiti eneo la magharibi mwa Libya.