Guterres aeleza wasiwasi wake kuhusu hali ya wahamiaji haramu huko Libya
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema kuwa amehuzunishwa sana kusikia taarifa ya kuaga dunia wahamiaji na wakimbizi wapatao 150 baada ya boti waliyokuwa wakisafiria kuzama katika pwani ya Libya juzi Alhamisi.
Farhan Haq Naibu Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameeleza kuwa Antonio Guterres amesikitishwa pia na ripoti kwamba manusura wengi wa ajali hiyo ya boti waliookolewa na kikosi cha ulinzi wa pwani ya Libya waliwekwa katika kituo cha kuwahifadhi wahajiri cha Tajoura kilichopo karibu na kambi ya jeshi ambacho tarehe Pili mwezi huu kililengwa na shambulio la anga. Wahajiri zaidi ya 50 waliuawa katika shambulio hilo.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesisitiza kuwa Libya si nchi salama kwa ajili ya kukimbilia hifadhi na kwamba wakimbizi wanapasa kuamiliwa kiutu na kwa heshima kwa mujibu wa sheria za kimataifa. Libya imekuwa ikitumiwa katika safari za maelfu ya wahamiaji haramu kuelekea Ulaya kutokana na nchi hiyo kuathiriwa na ukosefu wa amani na mapigano tangu mwaka 2011 baada ya kupinduliwa kiongozi wa nchi hiyo Kanali Muammar Gaddafi.
Wakati huo huo hali nzuri ya hewa imetajwa kuwa moja ya sababu zinazopelekea kuongezeka wimbi la wahamiaji haramu kuelekea Ulaya khususan wale wanaoanzia safari zao katika pwani ya magharibi mwa Libya.