Jeshi la Rwanda laingia Congo kusaka waasi wa Kihutu
Afisa mmoja wa jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo amesema kuwa wanajeshi wa Rwanda wameingia katika ardhi ya nchi hiyo.
Guillaue Ndjike Kaiko ambaye ni msemaji wa Operesheni ya Kijeshi ya Sokola-2 amesema wanajeshi wa Rwanda wameingia katika maeneo ya mashariki mwa Congo kwa ajili ya kusaka waasi wa Kihutu.
Watu walioshuhudia pia wamethibitisha kuwa mamia ya wanajeshi wa Rwanda wameingia mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Msemaji wa Operesheni Sokola-2 amesema kuwa wanajeshi wa Rwanda wanawasaka waasi walioko katika eneo la Buhumba huko mashariki mwa Congo.
Eneo la mashariki mwa Congo limekuwa likisumbuliwa na mashambulizi ya mara kwa mara ya waasi kutoka nchi jirani za Rwanda na Uganda.