Ghassan Salamé: Libya imekuwa uwanja wa vita wa nchi nyingine
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i55076-ghassan_salamé_libya_imekuwa_uwanja_wa_vita_wa_nchi_nyingine
Mjumbe maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Libya ametahadharisha kuhusu athari mbaya za vita katika nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika na kusema kuwa, Libya imekuwa uwanja wa vita wa nchi nyingine.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 29, 2019 22:33 UTC
  • Ghassan Salamé
    Ghassan Salamé

Mjumbe maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Libya ametahadharisha kuhusu athari mbaya za vita katika nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika na kusema kuwa, Libya imekuwa uwanja wa vita wa nchi nyingine.

 Ghassan Salamé amekiambia kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mjini New York kwamba, madola ya kigeni yanataka kuendelea vita na kuangamizwa kikamilifu nchi ya Libya kwa shabaha ya kufikia malengo yao.

Mjumbe wa Katibu Mkuu wa UN nchini Libya ameongeza kuwa, vita vya ndani nchini humo vimesababisha maafa ya binadamu katika maeneo mengi ya Libya na kuitumbukiza nchi hiyo katika matatizo mengi. Ghassan Salamé ametoa wito wa kusitishwa vita nchini Libya kwa mnasaba wa sikukuu ya Idi al Adh'ha.

Mapigano ya ndani Libya

Kundi linalojiita jeshi la taifa la Libya linaloongozwa na jenerali mstaafu Khalifa Haftar ambaye anaungwa mkono na kusaidiwa kwa miaka mingi na Saudi Arabia, Misri, Imarati na baadhi ya nchi za Magharibi, linadhibiti maeneo ya mashariki mwa Libya. Tangu tarehe 4 Aprili wapiganaji wa kundi hilo walianzisha mashambulizi makubwa kwa shabaha ya kuuteka mji mkuu wa Libya, Tripoli lakini wanakabiliana na upinzani mkali wa vikosi vya jeshi la Serikali ya Mwafaka wa Kifaifa inayotambuliwa rasmi na Umoja wa Mataifa. Mashambulizi hayo yameua zaidi ya watu elfu moja katika mji mkuu wa Libya, Tripoli na kujeruhi wengine wasiopungua 5500.

Libya ilitumbukia katika vita na machafuko ya ndani yaliyochochewa na nchi za kigeni na uingiliaji kati wa madola makubwa kama Marekani na baadhi ya nchi za Ulaya baada ya kuondolewa madarakani dikteta wa zamani wa nchii hiyo, Muammar Gaddafi mwaka 2011.