Waziri Mkuu wa Ethiopia atishia kukata moja kwa moja mawasiliano ya Intaneti
Waziri Mkuu wa Ethiopia ametangaza kuwa, endapo machafuko na hali ya kushajiishana wananchi kwa ajili ya machafuko itaendelea nchini humo, basi atachukua uamuzi wa kukata mawasiliano ya Intaneti kwa muda mrefu.
Waziri Mkuu Abiy Ahmed ameonya kuwa, kama machafuko yataendelea na kukawa na hali ya watu kushajiishana na kuhimizana kufanya machafuko kuputia mitandao ya kijamii, basi atakata mawasiliano ya Intaneti kwa muda mrefu.
Amebaiinisha kuwa, inachotaka serikali yake ni watu kutumia mawasiliano ya Intaneti kwa ajili ya ustawi na maendeleo na siyo kuhimizana kufanya machafuko.
Hayo yanajiri skiu chache tu baada ya Ethiopia kutangaza kuwa vikosi vya ulinzi na askari usalama wa nchi hiyo ndio watasimamia ulinzi na usalama katika mkoa wa kusini Sidama ulioathiriwa na machafuko nchini humo. Machafuko hayo hadi sasa yamesababisha kwa akali watu 20 kuupoteza maisha.
Itakumbukwa kuwa maandamano yaliibuka hivi karibuni wakati wanaharakati wa Sidama walipotaka kujitangazia eneo lao wenyewe. Kwa sasa Ethiopia ina maeneo tisa yanayojitawala yenyewe.
Kwa mujibu wa katiba ya Ethiopia, serikali kwanza inapasa kuandaa kura ya maoni kwa ajili ya kuruhusu kundi lolote la kikabila linalotaka kuunda eneo jipya lenye mamlaka yake. Kura hiyo ya maoni itaandaliwa baada ya kundi hilo kuwa limewasilisha ombi lake katika muda wa mwaka mmoja.