Aug 04, 2019 13:45 UTC
  • Niger yawatahadharisha raia wake na uharamia wa utekaji nyara wa Boko Haram

Viongozi wa serikali ya Niger wametoa indhari kwa raia wa nchi hiyo kujihadhari na uharamia unaofanywa na kundi la kigaidi la Boko Haram wa kuteka watu nyara na kudai kikomboleo cha fedha.

Viongozi wa Niger katika Manispaa ya Bosso wametangaza kuwa, ili kujipatia fedha, kundi la kigaidi la Boko Haram limeshadidisha vitendo vya utekaji nyara watu katika eneo hilo la kusini mashariki mwa nchi hiyo.

Mamadou Bako, Meya wa mji wa Bosso ambao hivi karibuni umeshuhudia matukio kadhaa ya utekaji nyara watu, amesema: Utekaji nyara huo umefikia kiwango cha kutia wasiwasi mkubwa kwa wananchi na viongozi wa mji huo na kwamba wanawake ndio walengwa wakubwa zaidi wa uharamia huo unaofanywa na magaidi wa kundi la ukufurishaji la Boko Haram.

Wanafunzi wasichana wa Nigeria, ambao waliwahi kutekwa nyara na kundi la kigaidi la Boko Haram 

Kwa mujibu wa viongozi wa Niger, vikomboleo vya fedha vinavyodaiwa na kundi la Boko Haram vimeifanya hali ya kiuchumi ya wakaazi wa baadhi ya maeneo ya nchi hiyo, ambao mapato yao ni duni, iwe mbaya zaidi.

Kuanzia mwaka 2015, kundi la kigaidi la Boko Haram limepiga kambi pia katika eneo la Diffa lililoko umbali wa kilomita 1500 kutoka mji mkuu wa Niger, Niamey.

Tangu mwaka 2016, hali ya hatari imetangazwa nchini Niger kutokana na athari za hujuma za kundi hilo la kigaidi, ambalo ngome yake kuu iko kaskazini mashariki mwa Nigeria.../

 

Tags