Kuruhusiwa Sheikh Zakzaky kwenda India; matunda ya juhudi za Waislamu wa Nigeria
Hatimaye juhudi za Waislamu wa Nigeria zimezaa matunda baada ya mahakama nchini Nigeria kuruhusu Sheikh Ibrahim Zakzaky, Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya nchi hiyo asafiri kuelekea nchini India kwa ajili ya matibabu.
Sheikh Zakzaky aliondoka jana mjini Abuja kuelekea India huku maafisa usalama wakiambatana naye katika safari hiyo.
Jumatatu iliyopita ya tarehe 6 Agosti, Mahakama Kuu ya jimbo la Kaduna ilitoa hukumu ya kuachiwa huru mwanaharakati huyo ili asafiri kuelekea nje ya nchi kwa ajili ya matibabu. Hivi karibuni serikali ya Nigeria ilitoa masharti mapya ya kwa ajili ya kutoa ruhusa hiyo.
Kamishna wa Usalama na Masuala ya Ndani wa Jimbo la Kaduna, Samuel Aruwan alinukuliwa na vyombo vya habari akisema kuwa, miongoni mwa masharti yanayopaswa kuzingatiwa kwa ajili ya kuruhusu safari hiyo ni Wizara ya Mashauri ya Kigeni kuainisha wakati wa kukutana na Sheikh Zakzaky hospitalini huko India na kadhalika kuarifisha wadhamini wawili mashuhuri.
Sheikh Ibrahim Zakzaky ambaye kutokana na harakati zake nchini Nigeria alikuwa chini ya mashinikizo ya vyombo vya usalama, Desemba 13, 2015 jeshi la nchi hiyo lilivamia na kufanya shambulio dhidi ya Huseinia ya Baqiyatullah katika mji wa Zaria na kufanya mauaji makubwa.
Siku hiyo askari wa jeshi la Nigeria waliwafyatulia risasi watu waliokuwa wamejumuika kwenye kituo hicho cha kidini na mbele ya nyumba ya msomi huyo na kuwaua shahidi mamia miongoni mwao wakiwemo watoto wake watatu wa kiume. Sheikh Zakzaky na mkewe walijeruhiwa vibaya kwa risasi katika shambulio hilo na kisha kutiwa mbaroni.
Tangu alipotiwa mbaroni, kiongozi huyo wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria kumekuwa kukifanyika juhudi kubwa za kutaka kuachiliwa huru mwanazuoni huyo kupitia mikusanyiko, maandamano na mashinikizo. Hata hivyo maandamano na mikusanyiko ya kulalamikia kuendelea kushikiliwa korokoroni Sheikh Zakzaky daima ilikuwa ikikabiliwa na ukandamizaji na mkono wa chuma wa vyombo vya usalama vya nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika. Ni hivi karibuni tu ambapo ofisi ya Rais Muhamadu Buhari iliitangaza Harakati ya Kiislamu ya Nigeria kuwa kundi la kigaidi na ikapiga marufuku shughuli za harakati hiyo.
Sheikh Zakzaky, akiwa Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu yya Nigeria amekuwa na nafasi muhimu katika miaka ya hivi karibuni ya kuleta mwamko miongoni mwa wananchi wa nchi hiyo hususan Waislamu akiwataka kusimama na kupinga dhulma.
Sheikh Abdalla Zengo, mmoja wa wanafunzi wa masomo ya dini na mwanaharakati wa haki za binadamu nchini Nigeria anasema kuhusiana na suala hilo kwamba, kabla ya Sheikh Zakzaky maulama na wasomi wote wa Kiislamu nchini Nigeria walikuwa kimya mbele ya dhulma na ukandamizaji; na mwanaharakati huyo ndiye aliyewaamsha wananchi na kuwaambia Waislamu kwamba, kwa mujibu wa mafundisho ya Qur'ani hawapaswi kudhulumu wala kuikubali dhulma.
Kwa upande mwingine matukio ya kisiasa na kubadilisha mwenendo na utendaji nchi kama Saudi Arabia na utawala haramu wa Israel katika miaka ya hivi karibuni na kugonga ukuta siasa zao katika eneo, kumezifanya tawala hizo zilizingatiie bara la Afrika na hivyo kufanya harakati za kuwa na ushawishi barani humo. Katika uwanja huo, Nigeria ikiwa nchi tajiri zaidi na yenye idadi kubwa zaidi ya watu baranii Afrika imekuwa mlengwa wa madola hayo. Tawala hizo zinafanya njama ambapo kupitia misaada yao ya kifedha na silaha ziwe na satua na ushawishi kwa siasa za viongozi wa Nigeria mkabala na Waislamu, na hivyo ziwe na taathira katika sera za kukabiliana na Waislamu katika nchi hiyo.
Muhammad Shueib Mussa, mhadhiri wa Chuo Kikuu anaashiria suala la jeshi la Nigeria kuwa chini ya udhibiti wa Marekani na hususan Israel na kwamba, watu wanaotaka kufikia vyeo vya juu wanapaswa kupata mafunzo huko Israel na kusema kuwa, lengo lao ni kutoa pigo dhidi ya Uislamu. Watawala wa Saudi Arabia na Marekani wanafanya njama za kuhakikisha kwamba, kunakosekana uhuru wa kidini nchini Nigeria na kisha kuzusha mifarakano katika nchi hiyo.
Licha ya mashinikizo yote, serikali ya Nigeria imetoa hukumu ya kuachiliwa huru kwa masharti Sheikh Ibrahim Zakzaky na kwa sasa msomii huyo yuko nchini India kwa ajili ya kufuatilia matibabu yeye pamoja na mkewe.
Licha ya kuwa kuachiliwa huru japo kwa masharti maalumu Sheikh Ibrahim Zakzaky unaweza kuhesabiwa kuwa ni ushindi kwa Waislamu wa Nigeria, lakini Waislamu hao wangali wana wasiwasi na hali ya kiafya ya kiongozi wao huyo pamoja na mwenendo wa matibabu yake hasa kwa kuzingatia kwamba, mara baada ya kuwasili nchini India, Marekani imetoa vitisho na mashinikizo kwa hospitali iliyompokea mwanazuoni huyo.
Inaonekana kuwa, Marekani na waitifaki wake wana kihoro na wahaka kutokana na Sheikh Zakzaky anavyopendwa na anavyokubalika, na hivyo wanafanya kila wawezalo kuweka vizingiti katika mchakkato wa matibabu yake. Hii ni katika hali ambayo, siyo Waislamu wa Nigeria tu, bali Waislamu wote ulimwenguni wanafuatilia kwa karibu mwenendo wa matibabu wa Sheikh Ibrahim Zakzaky na wanasubiria kwa hamu na shauku ili akamilishe matibabu yake na kurejea tena katika ulingo wa siasa nchini Nigeria.