Wasiwasi wa kuendelea kubanwa uhuru wa vyombo vya habari nchini Kongo
Shirika la Waandishi wa Habari Wasio na Mipaka limeelezea masikitiko yake kwa kuendelea kubanwa uhuru wa vyombo vya habari huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Mtandao wa habari wa Africa Time umenukuu taarifa ya taasisi hiyo inayojulikana kwa kifupi RSF ikisema kuwa, miamala jumla ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo inazidi kuporomoka hususan kuhusu uhuru wa vyombo vya habari na magazeti.
Shirika hilo limeongeza kuwa, kutiwa mbaroni kiholela, kupokonywa frikwensi na kutishwa waandishi wa habari ni katika mambo ambayo wanafanyiwa waandishi hao huko Kongo.
Shirika la Waandishi wa Habari Wasio na Mipaka limeongeza kuwa, serikali ya Kinshasa inavibana kupindukia vyombo vya habari na jambo hilo limepelekea kutoripotiwa vizuri matukio yanayojiri nchini humo hasa ya kisiasa.
Ikumbukwe kuwa wapinzani wa Rais Joseph Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wanamtuhumu rais huyo kuwa anafanya njama za kubadilisha katiba ili abakie madarakani kwa muda mrefu zaidi.
Kipindi cha uraia wa Joseph Kabila kinamalizika mwisho mwa mwaka huu.