Vita vya Libya vimesababisha watu 268,000 kuwa wakimbizi
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i55675-vita_vya_libya_vimesababisha_watu_268_000_kuwa_wakimbizi
Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa, vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Libya vimepelekea zaidi ya watu 268,000 kuwa wakimbizi.
(last modified 2026-03-27T07:58:19+00:00 )
Aug 29, 2019 23:07 UTC
  • Vita vya Libya vimesababisha watu 268,000 kuwa wakimbizi

Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa, vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Libya vimepelekea zaidi ya watu 268,000 kuwa wakimbizi.

Kwa mujibu wa  Ofisi ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNCHR) nchini Libya, kwa ujumla vita vya nchi hiyo vimepelekea watu 268,000 kuwa wakimbizi ambapo 120,000 miongoni mwao ni wakazi wa Tripoli ambao nyumba zao zimeharibiwa katika vita.

Taarifa hiyo imesema kuwa, watu wa Libya hivi sasa wanakumbwa na masaibu na matatizo makubwa  na kuna haja ya kuwapa misaada zaidi ya kibinadamu.

Ofisi ya UNCHR nchini Libya aidha imetoa taarifa na kusema watu wanaotoa misaada ya kibinadamu kwa wakimbizi na raia wengine wanakabiliwa na hatari ya kushambuliwa. Ripoti hiyo imesema kuwa katika kipindi cha siku 10 zilizopota wafanyakazi watatu wa kutoa misaada wameshambuliwa na kuuawa katika mji wa Benghazi.

Mashambulizi ya wanamgambo wanaojiita Jeshi la Kitaifa la Libya wanaoongozwa na jenerali muasi Khalifa Haftar yameshadidi katika mji mku Tripoli na kusababisha maafa makubwa. Wanamgambo hao wa Haftar wanapata himaya ya Saudi Arabia na Imarati. 

Kuanzi Aprili 4 mwaka huu, wapiganaji wa Haftar wamekuwa wakifanya mashambulizi kwa lengo la kuuteka mji wa Tripoli.

Waziri Mkuu Fayez al-Sarraj wa serikali ya Libya inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa.

Watu zaidi ya 1000 wameuawa katika mji wa Tripoli na wengine wasiopungua 5,500 wamejeruhiwa tangu kuanza mapigano kati ya pande mbili hizo. 

Ni vyema kuashiria kuwa, Libya ina serikali mbili hasimu, moja ikiwa na makao yake mjini Tobruk, iliyoko karibu na Jenerali Haftar, na nyingine ya Serikali ya Mapatano ya Kitaifa Libya inayoongozwa na Waziri Mkuu Fayez al-Sarraj inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa.

Libya ilitumbukia katika machafuko na vita vya ndani baada ya wanajeshi wa Marekani wakishirikiana na wale wa Shirika la Kijeshi la Nchi za Magharibi (NATO) kuishambulia nchi hiyo na kusaidia harakati za kumuondoa madarakani aliyekuwa kiongozi wa nchi Muammar Gaddafi hapo mwaka 2011.