Ugonjwa wa Chikungunya waenea Ethiopia, watu 15,000 waambukizwa
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i55685-ugonjwa_wa_chikungunya_waenea_ethiopia_watu_15_000_waambukizwa
Zaidi ya watu 15,192 wameambukizwa Chikungunya baada ya ugonjwa huu kuibuka katika mji wa mashariki wa Ethiopia Dire Dawa.
(last modified 2026-04-19T09:26:01+00:00 )
Aug 30, 2019 03:30 UTC
  • Ugonjwa wa Chikungunya waenea Ethiopia, watu  15,000  waambukizwa

Zaidi ya watu 15,192 wameambukizwa Chikungunya baada ya ugonjwa huu kuibuka katika mji wa mashariki wa Ethiopia Dire Dawa.

Mkurugenzi wa muda wa taasisi ya afya ya umma ya nchini Ethiopia Mesfin Wossen amesema hadi sasa hakuna kifo kilichoripotiwa, na sababu moja ni kwamba wagonjwa wamepata matibabu kwa wakati. Amewataka watu kusaidia kupuliza dawa ya mbu kwenye maeneo yenye tishio la Chikungunya mjini Dire Dawa, kuondoa maji yoyote ya mvua yaliyotuwama, na kufunika vitu vyote vya maji kwa vitambaa.

Dalili za ugonjwa huo ni pamoja na homa kali na maumivu ya viungo, misuli, kichefuchefu na uchovu.

Chikungunya ni ugonjwa unaoenezwa na mbu aina ya Aedes Egyptiae, Ugonjwa huu Hupelekea mtu kupata maumivu ya misuli, viungo  (joint) na homa kali.

Eneo la Dire Dawa katika ramani ya Ethiopia

Ugonjwa huu hauna tiba wala chanjo ,ila mgonjwa anaweza kupatiwa msaada wa kupunguza makali ya dalili za ugonjwa huu.

Kati ya njia za kukabiliana na ugonjwa huu ni kuzuia mbu kuingia nyumbani,  kuchunga mimea inayokua ndani ya nyumba isiwe na maji yaliyosimama na kufunika taka.

Katika miaka ya hivi karibuni ugonjwa wa Chikungunya umewahi kuripotiwa katika maeneo ya pwani ya Afrika Mashariki.