Magaidi wa kaskazini mwa Nigeria waua raia 11
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i55692-magaidi_wa_kaskazini_mwa_nigeria_waua_raia_11
Magaidi wa Nigeria wanaodhaniwa kuwa wanachama wa kundi la kigaidi la Boko Haram wameua raia wasiopungua 11 huko kaskazini mashariki mwa nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Aug 30, 2019 12:27 UTC
  • Magaidi wa kaskazini mwa Nigeria waua raia 11

Magaidi wa Nigeria wanaodhaniwa kuwa wanachama wa kundi la kigaidi la Boko Haram wameua raia wasiopungua 11 huko kaskazini mashariki mwa nchi hiyo.

Othman Ishaku Agahu ambaye ni mwanachama wa kundi linalosimamiwa na serikali ya Nigeria amesema kuwa, wahanga wa magaidi hao ni wafanyakazi wastaafu wa Idara ya Mawasiliano ya jimbo la Borno na walinyongwa katika shambulizi lililofanyika jana Alkhamisi. 

Afisa huyo amesema, kuna uwezekano mkubwa kwamba, mauaji hayo yamefanywa na wanachama wa kundi la kigaidi la Boko Haram.

Duru za hospitali ya eneo hilo zimethibitisha kuwa, maiti za raia 11 na majeruhi kadhaa zilifikishwa hospitalini hapo jana Alkhamisi. 

Ripoti kutoka Nigeria pia zinasema watu wengine 50 wakiwemo wanawake wajawazito na watoto wadogo walitekwa nyara Jumatano iliyopita na kundi la watu waliokuwa na silaha katika jimbo la Katsina.

Nigeria imekuwa katika hali ya tahadhari kubwa kutokana na kushadidi mashambulizi na hujuma za makundi ya watu wanaobeba silaha hususan katika maeneo ya kaskazini mwa nchi hiyo.